Dar, Kilimanjaro zatajwa kuongoza kwa utapiamlo

Muktasari:

Serikali imetoa tathmini ya lishe nchini huku utapiamlo ukionekana bado kuwa tatizo


Dodoma. Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imetaja mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro kuwa vinara wa utapiamlo wa lishe iliyozidi nchini.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TFNC, Geofrey Chiduo amesema hayo leo Jumanne Machi 19, 2019 jijini Dodoma wakati akizungumzia namna huduma za lishe zinavyoendelea nchini.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, baadhi ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wadau wa lishe.

Chiduo amesema kwa sasa wanapambana na maadui wawili ambao ni utapiamlo wa hali duni ya ukosefu wa virutubisho lakini kuna utapiamlo wa lishe uliopitiliza.

“Naomba nilitamke rasmi hapa kwa kuwa viongozi hapa mpo kwenye mikoa ya Dar es salaam na Kilimanjaro, suala la utapiamlo wa lishe iliyozidi wao ndio vinara,” amesema.

Amesema hata katika mikoa ambayo uzalishaji uko juu bado hali ya utapiamlo ipo juu na viwango katika mikoa vinatofautiana.

“Hata katika mikoa ambayo uzalishaji wa chakula ni mkubwa utapiamlo upo kiwango cha juu sana, hakuna  aliyesalama,” amesema.