Dar yaanza kunyunyizia viuadudu kudhibiti dengue

Muktasari:

Wakati wagonjwa wa homa ya dengue wakifikia 1,237, jiji la Dar es Salaam limeanza kunyunyizia dawa ya viuadudu (Biolarvicides) kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu wanaoeneza ugonjwa wa dengue ili kudhibiti ugonjwa huo, huku Serikali ikizitaka kaya moja moja kuua mazalia ya mbu waenezao ugonjwa huo na kuondoa maji yaliyotuama kwenye makazi yao.

Dodoma. Tahadhari zaidi imetolewa na Serikali kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuhusu homa ya dengue, huku baadhi ya halmashauri za jiji hilo zikianza kunyunyiza dawa za viuadudu (Biolarvicides) ili kupambana na mbu waenezao ugonjwa huo.

Imesema mpaka sasa jumla ya wagonjwa 1,237 wamegundulika kuwa na homa ya dengue, huku kati yao 1,150 ni kutoka Dar es Salaam, 86 Tanza na mtu mmoja kutoka Singida na vifo viwili.

Akizungumzia ugonjwa huo, Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Muhammad Kambi amesema takwimu za ugonjwa wa dengue kwa kipindi cha Januari hadi Aprili mwaka huu zinaonyesha idadi ya wagonjwa imefikia 1,237, vifo vya watu wawili lakini waliofariki pia walikua na maradhi mengine.

Hata hivyo, amelipongeza jiji la Dar es Salaam kwa kuanza kunyunyizia dawa viuadudu (Biolarvicides) kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu waenenezao ugonjwa huo ili kuudhibiti.

“Wizara inaelekeza mikoa na halmashauri zote nchini kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kufukia madimbwi ya maji, kunyunyizia dawa ya kuua viluwiluwi, kuondoa vitu vinavyosababisha mazalia ya mbu, kufyeka vichaka, kufunika mashimo ya maji taka kwa mifuniko pamoja kusafisha gata za paa la nyumba na kutoruhusu maji kusimama,” amesema.

Profesa Kambi amesema wizara ya afya kwa kushirikiana na mikoa na halmashauri zote nchini itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti ugonjwa huo kwa kuweka mpango wa dharura wa miezi sita kuanzia Mei mpaka Oktoba.