Dar yatumia asilimia 70 ya mkaa wote

Muktasari:

Katika mfululizo wa makala zetu kuhusu matumizi ya mkaa na mazingira, leo tunaendelea kuangalia jinsi ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa ulivyopoteza misitu mingi.

Dar es Salaam ni moja ya majiji yanayoendelea kukua kwa kasi, likiwa na watu wanaokadiriwa kufikia milioni tano, mzunguko mkubwa wa fedha na shughuli za kiuchumi.

Mambo hayo pia yanaambatana na ongezeko la matumizi ya mkaa ambayo yameifanya Dar es Salaam iwe kinara.

Jiji hili ni mtumiaji mkubwa wa mkaa unaotoka mikoa mbalimbali kulingana na upatikanaji wa nishati hiyo nyeti sehemu hizo. Hivyo mikoa inaipa Dar es Salaam mkaa wakati wote.

Wauzaji mkaa nao wanaona Dar es Salaam kuwa kimbilio lao; kuna wateja wa uhakika.

Licha ya kukua kwa teknolojia inayotoa nishati mbadala, bado wakazi wengi wa Dar es Salaam na maeneo mengine ya mijini wanaendelea kutumia mkaa kila siku kama nishati rahisi na nafuu.

Wananchi hao wanatumia mkaa kupika vyakula vyao vya kila siku kama vile maharagwe, makande, njugu mawe, chipsi na kuchemsha na kuchoma nyama.

Jiji la Dar es Salaam linatumia asilimia 70 ya mkaa wote wa Tanzania, likifuatiwa na majiji mengine ya Mwanza, Mbeya, Arusha na Tanga na pia maeneo mengine ya mijini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba anasema barabara nzuri na za uhakika zinazounganisha Dar es Salaam na mikoa mingine ni moja ya sababu inayochangia mkaa kuingia kwa gharama nafuu.

“Dar es Salaam ipo katikati ya mikoa inayozalisha mkaa hivyo kuwapa wasafirishaji unafuu wa kuleta mkaa bila kuingia gharama kubwa wakiwa na uhakika wa bidhaa hiyo kununuliwa,” anasema Waziri Makamba.

Anasema jiji hilo ni soko kuu la nishati hiyo na awali mkaa ulikuwa ukipatikana katika maeneo ya jirani yanayozunguka jiji ambayo ni  Bagamoyo na Kibiti kwa sababu ilikuwa nafuu kuusafirisha lakini sasa maeneo hayo hayatoshelezi mahitaji.

“Kadri muda unavyoenda, haya maeneo kwa sasa ni nadra kuchoma mkaa, ndio maana sasa hivi mkaa unatoka maeneo kama Morogoro, Pwani  na Tabora. Inatoka mikoa hii kwa sababu upatikanaji wake ni rahisi,” anasema Makamba.

Hata hivyo, Makamba anasema bado kuna changamoto katika kuzuia matumizi ya mkaa kutokana baadhi ya watu kutobadili tabia. Hawataki kuachana na matumizi ya nishati hiyo katika shughuli za upishi.

“Bado kuna dhana kwamba gesi siyo salama, ndio maana baadhi ya watu wanakaa mbali nayo wakihofia kulipukiwa. Lakini ukweli ni kwamba matukio ya gesi (kulipuka) ni machache sana,” alisema.

“Jingine ni gharama. Mkaa unaotokana na miti unatamba sokoni kwa sababu kuu tatu; bei ya mkaa huu inadhaniwa kuwa nafuu, pili, unapatikana kwa urahisi, kwenye mitaa ukitoka tu nje unakutana nao na unapatikana kwenye vipimo vya mauzo ambavyo wananchi wa kawaida wanaweza kuvimudu, unaweza kununua kuanzia Sh500 na hakuna nishati nyingine inayouzwa hivi ndio maana mkaa unatamba.”

Makamba  ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli, anasema mojawapo ya njia za kukabiliana na matumizi hayo ya mkaa unaotokana na miti ni kushindanisha bei ya mkaa mbadala na ule unaotokana na miti, lakini anasema suala hilo linahitaji nguvu ya Serikali kuingilia kati.

Matumizi ya mkaa mbadala

Makamba anasema mwamko umekuwa mkubwa wa watu kama wajasiriamali kujitokeza kubuni njia mbalimbali za kutengeneza mkaa mbadala ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana na miti.

“Hivi sasa watu wanazidi kupata ufahamu zaidi kuhusu mkaa mbadala ambao ni rafiki wa mazingira. Wajasiriamali katika tasnia hii wameongezeka zaidi huku mifumo ya masoko ya mkaa mbadala ikisambaa na bei yake ikiwa rahisi tofauti ule mkaa mwingine,” anasema.

“Tumeona kuna dalili nzuri na tukishikilia hapa matunda yataonekana. Kingine kizuri baadhi ya watu wanaotengeneza mkaa mbadala wameanza kupata tenda (zabuni) za kusambaza mkaa huu kwenye taasisi za umma na binafsi kama kambi za wakimbizi na za jeshi,” anasema Makamba.

Kuhusu taasisi za umma ambazo bado zinatumia mkaa, Makamba anasema Serikali inafikiria kutengeneza amri ya kiwizara kwa kutumia kanuni itakayoelekeza taasisi yenye watu zaidi ya 1,000 kuacha kutumia kuni na mkaa katika tarehe itakayotangazwa.

“Suala hili linakuja bado tupo katika mchakato wa kulifanyia kazi kwa sababu lazima tujue idadi ya taasisi hizi na uwezo wake,” anasema Makamba.

Hata hivyo, Makamba anasema suala la udhibiti wa ukataji wa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa linahitaji ushirikiano na si suala la wizara moja na kwamba hatua hiyo itasaidia jitihada za kuzuia matumizi ya mkaa unaotokana na miti.

Pia, Makamba anawataka wananchi ambao wapo karibu na maeneo ya misitu kuwa wakali na kuwazuia watu wanaoakata miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa badala kuwa watazamaji wakati uharibifu huo ukifanyika.

Mkurugenzi wa kampuni ya Kuja na Kushoka, inayojishughulisha na utengenezaji wa mkaa mbadala, Leonard Kushoka anasema ingawa teknolojia hiyo haijasambaa, amepata zabuni ya kuusambaza kwenye kambi za wakimbizi na magereza.

TFS wanasemaje

Mkurugenzi wa Idara ya Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Arjanson Mloge anasema mahitaji makubwa ya mkaa yametengeneza soko kubwa jijini Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na miji mingine.

Mloge anasema mkaa unaoingia Dar es Salaam ni magunia 500,000 kwa mwezi, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na timu ya TFS kati ya  Desemba, 2016 na Januari 2017.

“Kiasi hiki hakijumuishi mkaa unaoingizwa isivyo halali na bodaboda zinazokisiwa kuwa takribani 200 kwa siku. Mikoa inayoingiza kwa wingi mkaa jiji la Dar es Salaam ni Pwani, Tanga, Morogoro, Njombe (miti ya kupandwa), Lindi na Mtwara.

Wananchi wang’ang’ania mkaa

Pamoja na jitihada za kuzalisha nishati mbadala kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, wakazi wa Dar es Salaam wanaona mkaa haupekiki.

Mkazi wa Tabata Segerea, Jenista John anasema anatumia jiko la gesi na umeme lakini bado familia yake inatumia mkaa kutokana mazingira ya sasa.

“Nyumbani kwangu watu hawali chakula bila maharagwe, huo ni utaratibu wa kila siku mchana na usiku. Hivyo ninalazimika kununua mkaa kwa ajili ya kupikia vyakula kama hivi ambavyo haviwezi kuivishwa kwa gesi. Hata makande pia tunakula na hivyo kila wiki lazima nitumie mkaa,” anasema.

Mmoja wa wafanyabiashara wa mkaa, Martin Joseph anasema anauza mkaa kuanzia Sh1,000. Anasema kwa sasa bei imepungua na gunia moja linauzwa kati ya Sh35,000 na 40,000, wakati lile kubwa huuzwa kuanzia Sh45,000.

“Kushuka bei kunatokana na hali ya sasa si ya mvua, ni jua kali hivyo hata usafishaji wake unakuwa nafuu kutoka shambani. Nyakati za mvua gunia kubwa huuzwa hadi Sh60,000,” anasema Joseph.