Dawa ya ‘uzee’ yagunduliwa

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile (kushoto) akieleza jambo na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi (katikati) walipohudhuria kongamano la kimataifa lililokuwa likijadili kuhusu vinasaba nchini, lililofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Mratibu wa Taifa wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, Dk Liggyle Vumilia. Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Watu wazima sasa huenda wakawa na faida ya kubaki na ngozi zao za ujana licha ya kuwa na miaka mingi, hiyo ni baada ya kugunduliwa kwa tiba mpya inayotumia seli shina.

Mbali na kuzuia watu kuwa wazee pia seli hizo zina uwezo wa kutibu magonjwa sugu kama kupooza kwa muda mrefu, mtindio wa ubongo, selimundu, matatizo katika mfumo wa fahamu, kisukari na magonjwa mengine ya kijenetiki.

Seli shina ni chembechembe zenye uwezo wa kubadilika na kutengeneza kiumbe ndani ya mwili, katika nchi zilizoendelea zimeongezewa nguvu na kuanza kutumika kama tiba.

Akizungumza katika mkutano wa kwanza wa kimataifa wa afya kuhusu vinasaba, mwenyekiti mtendaji wa kampuni za Ipp, Regnard Mengi alisema matibabu hayo ya kisasa kupitia chembe zilizo ndani ya mwili wa binadamu zinaweza kumfanya mtu kuonekana kijana siku zote za uhai wake.

Pia, mbali na hilo alisema watoto wengi waliokuwa wakisumbuliwa na utindio wa ubongo wataweza kupata matibabu ya kina na kurudi katika hali zao za kawaida.

Awali, mkurugenzi wa Taasisi ya Neurogein inayohusika na ubongo na uti wa mgongo, Profesa Alok Sharma alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo nchini itakuwa ni ahueni kwa watu waliokuwa wakitumia muda mwingi kuuguza wagonjwa waliopooza viungo vya mwili na kushindwa kuwapeleka kufanyiwa matibabu India.

“Wapo ambao hawawezi kunyanyua mguu, mkono au wamepooza upande mmoja kupitia tiba hii watarudia hali yao ya kawaida na wale waliokuwa wakiwaangalia nyumbani kuanza kufanya kazi zao,” alisema Profesa Sharma na kuongeza: “Seli hizo hutolewa katika mwili wa mgonjwa na kufanyiwa maboresho kabla ya kurudishwa kwake kama tiba,”

Naye Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile aliitaka kampuni ya IPP Research, technology and Innovation Ltd kufanya kazi kwa kuzingatia miiko na kufuata vibali watakavyopewa siyo kinyume.

“Kuna watu huwa wanaomba vibali vya kufanyia utafiti suala fulani, wanafanya kitu kingine sasa hatutaki suala hili lijirudie kwenu na mfanye haraka ili tuweze kuwanufaisha wananchi wetu,” alisema.