Dawa ya mvua D’salaam ni ujenzi wa mifereji mipana

Msimu wa mvua huwa ni kero kubwa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam hasa wanaoishi mabondeni, wasafiri barabarani na wafanyabiashara.

Mvua zinazoendelea kunyesha zinaelezwa ni za wastani, lakini zinasababisha maafa kwa sababu ya miundombinu duni ambayo hairuhusu maji kutiririka kwa urahisi kwenda baharini au katika mito iliyopo katika jiji hilo

Tahadhari za mvua katika jiji hili zimekuwa zikitolewa kila mwaka lakini wananchi wamekuwa wakipuuzia tahadhari hizo kwa kuhama maeneo yao kwa muda kisha kurejea tena baada ya mvua kupungua.

Mei 10 mwaka huu, meneja wa kituo kikuu cha utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Samwel Mbuya alisema mvua za mfululizo katika baadhi ya maeneo ya Pwani ya Kaskazini (mikoa ya Tanga, Dar es salaam na Pwani pamoja na Unguja na Pemba), zinatarajiwa kuendelea kwa siku mbili mpaka karibu na katikati ya Mei. Awali TMA ilisema mvua hizo zingeisha Mei 12.

Hata hivyo, alisema vipindi vya mvua za mfululizo vinatarajiwa kujirudia kuanzia katikati ya mwezi huu. Alitoa angalizo kwa wananchi kuchukua tahadhari kwa sababu hata mvua ndogo zinaweza kusababisha madhara.

“Pamoja na kwamba mvua za masika zinatarajiwa kupungua katika maeneo mengi mwishoni mwa mwezi huu, athari za mvua kubwa zilizonyesha katika kipindi cha wiki moja mfululizo katika ukanda wa Pwani ya Kaskazini pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, zimesababisha kutuama kwa maji na mafuriko.

“Hivyo, kutokana na ardhi kuwa na unyevunyevu mwingi, ongezeko kidogo la mvua linaweza kuendelea kusababisha athari kama zilizokwisha jitokeza,” alisema Mbuya wakati akitoa taarifa kwa umma mwishoni mwa wiki iliyopita.

Athari ya mvua

Athari zilizojitokeza katika mvua zilizonyesha wiki iliyopita ni pamoja na miundombinu ya barabara kujaa maji kutokana na mifereji kujaa maji. Jambo hilo limesababisha msongamano mkubwa wa magari barabarani na baadhi ya maeneo magari kuharibika kwa kutumbukia mitaroni.

Mfano mzuri ni Barabara ya Morogoro katika eneo la Jangwani ambalo linajaa maji kila mvua zinaponyesha.

Barabara katika sehemu hiyo hufungwa kwa muda kutokana na mafuriko kuhatarisha maisha ya watu na mali zao wanapopita katika eneo hilo.

Mei 13, kampuni ya UDA-RT ilisitisha huduma zake za usafiri kwa mabasi yanayotumia barabara hiyo kwa sababu ya kujaa maji. Jambo hilo lilisababisha usumbufu kwa abiria hasa wanaoishi Mbezi na Kimara kwa sababu wanategemea usafiri huo.

Wataalamu watoa kilio

Wataalamu wameilalamikia Serikali kwa kushindwa kuboresha miundombinu ya maji ya mvua kwa sababu ndiyo chanzo kikubwa cha mafuriko yanayotokea katika jiji hili. Wamesema mifereji mipana ikijengwa itasaidia kupunguza mafuriko.

“Serikali za mitaa kwa maana ya manispaa za Ilala, Kinondoni, Ubungo na Temeke zina wajibu wa kujenga mifereji mipana kwenye maeneo yao hasa pale Jangwani. Tatizo la Dar es Salaam linajulikana kuwa ni miundombinu lakini hatuoni kinachofanyika, mifereji inayojengwa ni ya kawaida ambayo haifai kwa hali tuliyonayo hapa,” anasema mhandisi wa kampuni ya B&J Engineering Co Ltd, Samson Buberwa.

Mhandisi huyo anabainisha kwamba ili kukomesha mafuriko katika jiji la Dar es Salaam, ni vema serikali ikawekeza kwenye mradi mkubwa wa kutengeneza mifereji mipana ambayo itakusanya maji yote mitaani na kuyaelekeza baharini.

Aprili 2018, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo aliliambia Bunge wakati akiwasilisha hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2018/19 kwamba mradi wa bonde la Msimbazi utatekelezwa kwa Dola za Marekani 20 milioni (Sh45 bilioni).

“Serikali inaendelea na usanifu wa mradi wa Bonde la Mto Msimbazi unaofanywa na kampuni mbili COWI Tanzania Ltd na Ecorys ya nchini Netherland ili kupata mkandarasi wa kujenga na kuboresha miundombinu ya bonde hilo,” alisema Jafo.

Alisema kazi ya usanifu ilipangwa kukamilika ifikapo Juni 2018 na kwamba mradi huo ulikuwa ni mkakati wa kupunguza athari za mazingira na mafuriko katika bonde la Mto Msimbazi. Alibainisha kwamba mradi huo ungetekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka Shirika la DFID.

Hata hivyo, mpaka sasa ujenzi wa mradi huo bado haujaanza huku mafuriko yakiendelea kuwasumbua wananchi wa Dar es Salaam na kuharibu mazingira ikiwemo mmomonyoko wa udongo na kusafirisha takataka kwenye makazi ya watu.

Alipoulizwa kuhusu maendeleo ya mradi huo, Naibu Waziri wa Tamisemi, Josephat Kandege alisema mradi huo unaendelea vizuri lakini haukuanza kama ulivyopangwa kwa sababu kuna taratibu ambazo zinafuatwa ili wafadhili waweze kutoa fedha.

“Hii miradi ambayo tunategemea fedha za mkopo ina taratibu zake, lazima tufuate taratibu zote kama kuna watu wanaotakiwa kulipwa fidia basi tuhakikishe wanalipwa. Kwa sasa niseme mradi huo unaendelea vizuri,” anasema Kandege.

Wakazi wa Dar es Salaam wameitaka serikali kuimarisha mifereji hasa pembezoni mwa barabara zinazojengwa ili maji yapate njia pana ya kupita. Wamesema hali hiyo itapunguza athari kwa maeneo ya mabondeni, pia kulinda miundombinu ya barabara isiharibiwe na maji.

“Kila mwaka wanatuambia kwamba watajenga mtaro mkubwa hapa Jangwani lakini hatuoni chochote kinachofanyika. Hapa tunataka daraja kubwa na mfereji mpana unaokwenda baharini,” anasema mkazi wa Jangwani, Salum Mrisho.

Mwananchi mwingine, Flora Mwembezi anasema athari za mafuriko kwa Dar es Salaam siyo kwa wakazi wa mabondeni pekee bali kwa kila mwananchi kwa sababu mafuriko hayo yanaharibu barabara au kufunga njia na kusababisha kero ya usafiri kwa wananchi.

“Sisi tunaotumia daladala ndiyo tunaumia zaidi, tukiambiwa barabaraba imefungwa tunalazimika kutembea kwa miguu huku tunayeshewa. Serikali ijenge mifereji kama ile ya barabara ya Mandela,” anasema mkazi huyo wa Ubungo.