Dawa za bei nafuu kutibu NCDs mbioni

Thursday March 21 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi hmak[email protected]

Kampala, Uganda. Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya afya ipo katika majadiliano na kampuni ya utafiti wa dawa ya Novartis kwa ajili ya kuisambazia dawa za kutibu magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) zitakazouzwa kwa gharama nafuu.

Dawa hizo zitakazouzwa kwa gharama ya dola moja ya Marekani kwa pakiti ya vidonge 100 ni zile zinazotibu saratani, presha na magonjwa mengine yasiyoambukiza.

Mpango huo unafanywa kwa nchi za kipato cha kati na chini ili kuhakikisha upatikanaji wa dawaunakuwa kwa bei rahisi.

Hayo yamesemwa na mkuu wa kampuni ya Novartis Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, Dk Nathan Mulure leo katika mahojiano maalum na Mwananchi wakati wa kongamano lililojadili afya kwa wote lililojikita zaidi kuzungumzia magonjwa yasiyoambukiza, jijini Kampala.

Dk Malure ameeleza mpango huo unatarajiwa kuanza Juni mwaka huu.

“Mpaka sasa majadiliano na makubaliano yanakamilika na tunatarajia kuanza kusambaza huduma ili kurahisisha dawa za kutibu magonjwa yasiyoambukiza kufika Tanzania na hivi sasa bado tupo kwenye mazungumzo na wizara pamoja na taasisi zinazosimamia hospitali binafsi Tanzania kuona ni namna gani huduma hii itawafikia,” amesema.

Advertisement

Akizungumzia suala hilo, mkurugenzi mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD), Laurean Bwanakunu amesema wanataka kuingia nao mkataba mkubwa zaidi kwa kuwa wamepanga kuwauzia kwa bei ya dola moja kwa kila dawa.

“Ni rahisi unaponunua dawa nyingi kwa dola moja ni kama Sh 2,000 hivi na ni pakiti nzima ya vidonge 100 tupo kwenye makubaliano na nchi nyingi zimefanya hivyo.”

“Tumekubaliana na wizara ya afya wanaliangalia hilo waone kama tutaweza kuingia mkataba huo na wakishafanya makubaliano sisi tutaanza kununua dawa, tutaingia nao mkataba tofauti na wa awali kwani baadhi ya dawa tunanunua kwao,” amesema.

Mpaka sasa nchi mbalimbali Afrika ikiwamo Cameroon, Nigeria, Kenya, Uganda, Rwanda na Ethiopia zimefikiwa na programu hiyo na kusaidia kuondoa gharama kubwa zilizotumika kutibu magonjwa hayo.

Mkurugenzi mtendaji mkuu wa shirika la Amref Africa, Dk Githinji Gitahi amesema ni wakati muafaka sasa kila nchi kuamua kuwa afya kwa wote si ya kuchagua bali ni lazima na haki.

Advertisement