Dereva kortini kukatisha ruti

Muktasari:

Alidai dereva huyo aligeuza gari maeneo ya Mikunguni kitendo ambacho ni kosa kisheria na baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa alikiri na kuiomba Mahakama imsamehe akijitetea kuwa ndiyo kosa lake la mwanzo.

Unguja. Dereva Abdallah Mkubwa Khatib (29) mkazi wa Mwanakwerekwe wilaya ya Magharibi ‘B’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, amejikuta akipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo ya wilaya hiyo kwa tuhuma ya kutomfikisha abiria wake hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.

Akisomewa hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Mohammed Ali Haji, mwendesha mashitaka wa polisi, Fadhila Omar alidai dereva huyo alikatisha ruti ya njia ya kwenda hospitalini hapo kinyume cha kifungu cha 78 na kifungu 205 (2) (b) na kifungu cha 201 (1) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 ya Zanzibar.

“Machi 13 mwaka huu majira ya saa 5:25 asubuhi maeneo ya Mikunguni wilaya ya Mjini mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, mshitakiwa akiwa dereva wa gari inayofanya safari zake za kubeba abiria katika njia 510 akitokea Kibandamaiti kuelekea Mfereji wa Wima alikamatwa baada ya kukatisha ruti na kutofika Darajani kama inavyotakiwa,” alidai.

Alidai dereva huyo aligeuza gari maeneo ya Mikunguni kitendo ambacho ni kosa kisheria na baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa alikiri na kuiomba Mahakama imsamehe akijitetea kuwa ndiyo kosa lake la mwanzo.

Upande wa mashtaka ulieleza kuwa hauna kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshitakiwa huyo mahakamani hapo.

Hata hivyo, Hakimu Mohammed alimtia hatiani mshitakiwa huyo na na kumpa adhabu ya kulipa faini ya Sh40,000 na akishindwa atakwenda kutumikia kifungo cha mwezi mmoja jela ili iwe fundisho kwake na kwa madereva wengine wanaodharau sheria za barabarani.

Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo na kunusurika kwenda gerezani.