Dhahabu yakamatwa Handeni ikitoroshwa

Muktasari:

  • Gramu 187 za dhahabu  zinazokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya  Sh13 milioni zimekamatwa na kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo mkoa wa Tanga katika mgodi wa dhahabu wa Magambazi

Handeni. Gramu 187 za dhahabu zinazokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya  Sh13 milioni zimekamatwa na kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo mkoa wa Tanga katika mgodi wa dhahabu wa Magambazi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Godwin Gondwe ambaye ni mkuu wa wilaya hiyo amesema wahusika walifanya uchenjuaji madini hayo bila kufuata taratibu.

Amesema polisi wanamshikilia mkuu wa kambi ya machimbo ya dhahabu ya Magambazi kwa tuhuma ya kushindwa kutoa taarifa kwenye vyombo husika wakati uchenjuaji dhahabu ukifanyika licha ya kufahamu taratibu.

 “Hii ni dalili ya kutaka kutorosha madini haya. Taratibu za madini zinaeleza wazi kuwa wakati wa uchenjuaji katika hatua za mwisho wanatakiwa kuishirikisha kamati ya ulinzi na usalama lakini hawakufanya hivyo,” amesema Gondwe.

Kaimu ofisa madini mkazi mkoa wa Tanga,  Nicas Sangaya amesema walipata taarifa madini hayo yanataka kutoroshwa na baada ya kufuatilia walibaini ni kweli.

Amesema walikwenda eneo husika na kuwakamata kutokana na kukiuka taratibu zote za kuchenjua madini.

“Thamani ya madini haya ni zaidi ya Sh13 milioni, ni gramu 186.9. Tutayachukua madini haya na kuyapeleka ofisi za Benki Kuu (BoT) tawi la Arusha  kwa ajili ya kuhifadhiwa kama taratibu zinavyoelekeza,” amesema Sangaya.

Serikali iliwaondoa wachimbaji wadogo katika mgodi wa Magambazi Novemba 2016 na kukabidhiwa kampuni ya uchimbaji madini ya Canaco.