Diamond adhihirisha ufalme wake Kahama, amwaga noti kwa mashabiki

Muktasari:

Atua na helkopta, mashabiki wapagawa kwa noti  alizomwaga barabarani

Kwa zaidi ya saa 24 mji wa Kahama, Shinyanga umetawaliwa na mwanamuziki Diamond Platnumz ambaye leo atafanya onyesho lake la One Mic, One Man katika uwanja wa mpira wa Kahama.

Katika maeneo mbalimbali ameonekana akifuatwa na msafara wa bodaboda, bajaji, magari na waendao kwa miguu wakimshangilia huku wakisema ‘Simba’, ‘Simba’, ‘Simba’.

Jana aliwasili katika mji huo kwa usafiri wa helkopta na kutua katika Kijiji cha Masumbwe ambapo alilakiwa na mamia wa mashabiki.

Katika kusherehesha mkusanyiko huo, Diamond alifungua burungutu la noti na kuanza kuzimwaga kwa mashabiki hali iliyougeuza eneo hilo kufunikwa kwa vumbi kutokana na mashabiki kuzirukia kila mmoja akijaribu bahati yake.

Mwanamuziki huyo anayetamba na wimbo Inama, katika Uwanja wa Kahama jana alimwaga noti kwa mashabiki waliofika kumshuhudia ikiwa ni  takribani saa 24 kabla ya onyesho lake hilo la kwanza katika Mji huo katika kipindi cha miaka saba.

Meneja wa mwanamuziki huyo, Babu Tale amesema WCB ilitenga fedha nyingi kwaajili ya onyesho hilo na lengo kubwa likiwa ni kurudisha shukrani kwa jamii.

Amesema mbali na fedha zilioonekana wazi, Diamond ametoa misaada ikiwamo katika kituo kinacholea watoto wenye ualbino, Buhangija.

“Ukipiga hesabu za kila kitu tulichofanya tangu mwanzo mpaka sasa unaweza kuta inafika Sh100 milioni  lakini hilo sio muhimu kwetu, kikubwa ni kurudisha fadhila kwa jamii ambayo imemuunga mkono msanii wetu miaka mingi,” alieleza.

Diamond pia aliandaa futari maalumu jana jioni ambayo iliwakutanisha watu mbalimbali katika mji huo.