Dk Abbas asema sekta ya madini Tanzania imeonyesha mwanga

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara Habari maelekezo Dk Hassan Abbas akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo

Muktasari:

  • Mageuzi yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania katika sekta ya madini yamebadili mwelekeo wa sekta hiyo na kuingiza fedha nyingi

Dar es Salaam. Serikali imesema Sh302. 63 bilioni zimekusanywa katika sekta ya madini kuanzia Julai Mosi, 2018 hadi sasa, kiasi  ambacho hakijawahi kukusanywa katika sekta hiyo.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Mei 30, 2019 na msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas katika mkutano wake na waandishi wa habari, akibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na mageuzi yaliyofanywa na Serikali iliyopo madarakani.

Amesema mabadiliko hayo yameipa heshima Tanzania na kuifanya kuwa mfano kwa nchi ya Afrika katika kuwabana wanyonyaji walioweka mizizi kwenye sekta hiyo.

“Watafiti wengi wanafanya tafiti kujua ni namna gani Tanzania imefikia hatua hiyo. Kuna nchi nyingi zimeanza kufuata nyayo zetu kwa kifupi tumejiwekea heshima kubwa,” amesema Dk Abbas.

Amesema siri kubwa ya mafanikio hayo ni kuongeza usimamizi, ufuatiliaji na kuwekwa mifumo ya kisayansi.

Licha ya kuanzishwa ndani ya muda mfupi masoko ya madini katika mikoa mbalimbali nchini yametajwa kuwa na mchango mkubwa katika sekta hiyo na kuzuia mianya ya utoroshaji wa madini vitendo vilivyokuwa vinaminya mapato ya Serikali.

Kuhusu mfumo wa kufuatilia mawasiliano ya simu na miamala ya fedha (TTMS), Dk Abbas amesema umeonyesha mafanikio kwani tangu kuanza kwake umeingiza Sh97.16 bilioni fedha ambazo Serikali ilikuwa haizipati awali.