Dk Bashiru: CCM kuendesha kampeni za chaguzi zijazo kistaarabu

Muktasari:

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amezungumzia chaguzi mbili zinazokuja nchini zitafanyika kwa nidhamu ya hali ya juu

Dodoma. Katibu Mkuu wa CCM, Dk  Bashiru Ally amesema wataendesha kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa na ule mkuu kwa ustaarabu na kwa kufuata sheria.

Dk Bashiru amesema hayo leo Jumamosi Machi 23, 2019 wakati akizindua mkakati wa kukomaza demokrasia katika ngazi ya mashina ulioandaliwa na CCM mkoa wa Dodoma.

Amesema msimu wa uchaguzi unaelekea kuanza na kwamba uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2019 na uchaguzi mkuu 2020 ni chaguzi za kwanza kufanyika chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania, John Magufuli.

“Matarajio yetu ni kwamba kama alivyosimamia nidhamu ndani ya chama chetu na ndani ya Serikali, atafanya hivyo kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu ujao unafanyika kwa amani na nidhamu ya hali ya juu,” amesema.

Amesema yeye kama mtendaji mkuu wa chama anaahidi kwa umma kuwa wanachama wao wataendesha kampeni kwa namna ya ustaarabu, watafanya siasa kwa kuvumiliana, kuheshimiana na kwa kufuata sheria.

“Kwa hiyo wanaojiandaa kufanya chokochoko, wanaota balaa liangukie nchi hii washindwe na walegee,” amesema.

Amesema ni lazima nchi itawalike na shughuli ya maendeleo ya wananchi lazima zifanyike kwa mtindo wa haki.