Dk Bashiru: Nape anahitaji kupikwa

Friday April 26 2019

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bshiru Ally amesema licha ya kuwa Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ni kiongozi mzuri na alikuwa mwenezi wa CCM lakini bado anahitaji kupikwa.

Ameyasema hayo leo Aprili 26, 2019 alipokuwa anahojiwa na Tido Mhando katika kipindi cha Gumzo la Uchaguzi kilichorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC 2)

Akijibu swali aliloulizwa na mtangazaji Tido Mhando juu ya kuwepo kwa wabunge walio na kauli kali kama wanatia wasiwasi katika chama huku akiwatolea mfano mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye.

Akijibu swali hilo Dk Bashiru alisema

“Nape ni Mwenezi wetu, jasiri kabisa lakini anahitaji kupikwa. Nilichokuwa nasema siyo nakubali kila kitu bali mtambue kuwa chama kinawajibu wa kuwasikiliza, kuwaandaa, kuwaamini na kuwasimamia kama wanakwenda inavyotakiwa.”

“Lakini kwa jinsi hali ilivyo ni kati ya watu ambao wana mchango mkubwa na ndiyo maana nimeomba chama tujenge chuo cha kuandaa viongozi kutoka nchi sita tofauti ili tuweze kuandaa viongozi waliochipukia kwa sababu suala hili linahitaji maarifa na bila shaka tutakuwa na kina Nape na Bashe wengi,” amesema Dk Bashiru.

Dk Bashiru amesema wakati Nape na Bashe wanateuliwa kugombea nafasi za ubunge wakitokea umoja wa vijana kwa wakati huo UVCCM ulikuwa umegeuzwa kuwa kituo cha wagombea kujipima umaarufu wao.

“Kutokea umoja wa vijana wakaaminiwa wakapewa nafasi za uongozi hivyo ule udadisi ukaonekana kuwa na ujasiri ndani yao,” amesema Dk Bashiru

Advertisement