Dk Bashiru: Nimeota ndoto mbaya kwa viongozi wa Wizara ya Kilimo

Muktasari:

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewaonya viongozi wa Wizara ya Kilimo akisema kuna jambo baya litawapata iwapo hawasimamia vyema maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa.

Mwanza. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewaonya viongozi wa Wizara ya Kilimo akisema kuna jambo baya litawapata iwapo hawasimamia vyema maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa.

Dk Bashiru alitoa kauli hiyo jana katika ziara yake ya kukagua miradi na maendeleo ya chama hicho tawala mkoani Mwanza akisema ameota ndoto mbaya iwapo viongozi wa wizara hiyo watashindwa kusimamia vyema vyombo vitatu vya maendeleo ya kilimo vilivyopo chini yao.

Alivitaja vyombo hivyo kuwa ni bodi za mazao, tume ya ushirika na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji alizosema hazijafanya vya kutosha kusaidia sekta ya kilimo aliyosema ndivyo imebeba ufanisi kwenye ajenda ya Tanzania kuwa Taifa lenye uchumi wa kati kufikia mwaka 2025 kupitia mapinduzi ya viwanda na maendeleo ya sekta ya kilimo.

Bila kufafanua mchakato aliosema unaendelea, alihoji ni nani anayekwamisha mchakato wa kubadilisha sheria na sera ya kilimo ili kuunganisha bodi na vyombo vya kusimamia maendeleo ya mazao ya kilimo.

“Kila zao limewekewa bodi. Kuna Bodi ya Miwa, Bodi ya Sukari, Bodi ya Tumbaku, Bodi ya Pamba, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Pareto, Bodi ya Chai, Bodi ya Korosho bodi, Bodi ya Kusimamia Mazao ya Kimkakati na hii Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko. Tunataka utitiri huu wa bodi za kinyonyaji uondoke kwa kuziunganisha. Hilo wazo lipo wizarani linachakatwa; mchakato huo ukamilike tuwe na vyombo viwili vya mazao. Bodi ya mazao mchanganyiko na Bodi ya Mazao ya Kimkakati,” alisema Dk Bashiru.

Alisema katika nchi maskini kama Tanzania inayoamini falsafa ya Siasa ni Kilimo, ni muhimu kusimamia vyema vyombo vinavyosimamia majukumu ya kisheria na maendeleo ya sekta ya kilimo.

“Nimezungumza na waziri wa kilimo na katibu mkuu. Wamenijulisha mchakato wa kubadilisha sheria na sera ya kilimo kuunganisha vyombo vya usimamizi. Najiuliza nani anasababisha kujivutavuta, ana lengo gani na ametumwa na nani?”

“Matatizo yakitokea kwenye mazao hayo, CCM ndiyo inasulubiwa. Kama jambo hili linaendelea kuwa la kuchakatachakata na mchakato haukamiliki; CCM tukiingilia tutawachakata wanaotuchelewesha,” alisema.

Dk Bashiru alitembelea ofisi ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ukiliguru wilayani Misungwi, kushiriki kikao cha kamati ya siasa za wilaya za Nyamagana na Ilemela.