Dk Bashiru: Nyerere angerudi angefurahi kuona Muungano upo imara

Muktasari:

  • Katibu mkuu wa CCM Dk Bashiru Ally amesema endapo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere angefufuka angefurahi kuona Muungano bado unadumu na nchi bado ina utulivu wa kisiasa

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ametaja mambo mawili ambayo iwapo Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere angerudi angefurahia na matatu ambayo yangemsikitisha.

Mambo ambayo angefurahia ni kuona Muungano bado upo imara na utulivu wa kisiasa lakini angepata simanzi baada ya kuona bado Waafrika hawajapata nafasi ya kuzungumza kuhusu umoja wao, ubaguzi uliopo Afrika Kusini na jinsi Tanzania ilivyoshindwa kuinua kilimo. 

Ameyasema hayo leo Aprili 26, 2019 alipokuwa akihojiwa na Tido Mhando katika kipindi cha Gumzo la Muungano kilichorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC 2)

“Angefurahia kuwepo kwa miaka 55 ya Muungano, hii ni kwa sababu walikuwepo watu waliokuwa na nia ya kuvunja Muungano huu lakini alisimama na kuhakikisha kuwa suala hilo halitokei na alipata kazi kubwa katika kujenga amani na umoja wa nchi,” amesema Dk Bashiru.

Dk Bashiru amesema angesikitishwa namna Sudan inavyosambaratika, kwa kugawana vipande na kufanya kuwa mataifa mawili yaani Sudan Kusini na Sudan, pia machafuko yaliyopo katika nchi za Libya na Somalia.

“Hali ilivyo hivi sasa Afrika Kusini nchi ambayo Waafrika wenyewe walipaswa kushirikiana baada ya uhuru na badala yake wanafukuzana haya ni mambo yanayoumiza sana kwa sababu, Afrika ni moja,” amesema Dk Bashiru.

Kwa upande wa Tanzania angesikitika kuona jinsi gani mchango wa kilimo bado ni mdogo kwa sababu yeye alikuwa akiamini kuwa siasa ni kilimo.

“Nyenzo zetu za kilimo bado ni duni, hatuna uwezo wa kumwagilia wakati hali ya hewa inabadilika, hatuna uhakika wa usalama wa chakula chetu na tumeshindwa kuimarisha ushirika japo hata yeye alishindwa,” amesema Dk Bashiru.