Dk Bashiru: Sijafurahia utendaji wa mkurugenzi Wilaya ya Rombo

Muktasari:

Katibu Mkuu wa CCM amesema viongozi wanawake katika mkoa wa Kilimanjaro,wanafanya kazi nzuri lakini hajafurahishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo.


Same. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema utendaji kazi wa mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Magreth John haujamfurahisha.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 10, 2019 wakati akizungumza kwenye kikao kilichofanyika katika jimbo la Same Mashariki na kuwakutanisha viongozi wa chama hicho tawala na Serikali ya Tanzania.

"Jana nilikuwa Rombo mkurugenzi hakunifurahisha nimeacha ujumbe ajifunze kwa wenzake kwa kuwa natambua wanawake viongozi Kilimanjaro wanachapa kazi na mko vizuri lakini msibweteke.”

"Katika Mkoa wa Kilimanjaro tunao viongozi wanawake, mkuu wa Mkoa, wakuu wa wilaya, katibu wetu wa wilaya ni mwanamke na pia kuna wabunge watatu wanawake na wote wameniridhisha yule wa Rombo ni mwanamke ila hajanifurahisha,” amesema Bashiru.

Amewataka viongozi wanawake kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa kuwa utendaji wao ni mzuri.

Dk Bashiru pia amewaonya watumishi wa chama hicho wanaotumia magari ya chama katika shughuli binafsi, kwamba watakaobainika hawatavumiliwa.