Dk Bashiru aibua mjadala

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally

Muktasari:

  • Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi jana, baadhi ya wachambuzi na watetezi wa haki za binadamu walimpongeza Dk Bashiru kwa kauli hiyo.

Dar es Salaam. Kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ya kutahadharisha dhidi ya machafuko kutokana na uvunjifu wa haki na usawa imeibua mjadala miongoni mwa wanaharakati na wachambuzi wakitaka hatua zaidi zichukuliwe hasa katika haki ya kufanya siasa nchini.

Akizungumza juzi mjini Morogoro katika kongamano la kumbukumbu ya waziri mkuu wa zamani, Edward Sokoine, Dk Bashiru alitoa mfano wa malalamiko ya madereva wa bodaboda kuhusu manyanyaso wanafanyiwa na polisi na kusema hicho kinaweza kuwa chanzo cha machafuko.

Akitoa mifano ya machafuko yaliyotokea Tunisia na Libya, Dk Bashiru alisema viongozi wanaokiuka usawa na haki hubaki wapweke na matokeo yake hutawala kwa mabavu, jambo ambalo alisema Sokoine hakuwa hivyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi jana, baadhi ya wachambuzi na watetezi wa haki za binadamu walimpongeza Dk Bashiru kwa kauli hiyo.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa alitoa mifano ya nchi zilizoingia kwenye machafuko akisema waliosababisha ni watu wasiotarajiwa kabisa.

“Umeona Sudan, siyo mpaka watu wengi waungane ndiyo walete machafuko, au siyo mpaka vyama vikubwa vya siasa kama CUF, Chadema na ACT Wazalendo waungane. Anaweza kutokea mtu asiyejulikana kama ilivyotokea Tunisia.”

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema ana mwunga mkono Dk Bashiru kwa kauli yake ya usawa na haki kwa wananchi.

Mwanasiasa mkongwe, Njelu Kasaka alisema haki imekuwa ikivunjwa hasa katika haki ya kujumuika na kufanya siasa.

Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe alisema: “Ukiukwaji wa haki za raia ni pamoja na raia kukosa haki za kisiasa kama vile uhuru wa kujiunga na vyama na vyama kufanya siasa kwa uhuru. Haki za kisiasa na kiuchumi kote duniani zimekuwa chanzo kikubwa cha vurugu,”

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Ahmed Msangi alipoulizwa kuhusu ukandamizwaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na jeshi hilo, alisema hawezi kuzungumza kwa kuwa yuko likizo.

Hata hivyo, Katibu wa NEC wa Siasa na Uhusiano na Kimataifa wa CCM, Kanali Ngemela Lubinga alisema jitihada zinazofanywa na Serikali ni kuhakikisha watu wanatendewa haki.

“Katibu mkuu anachosema jitihada hizo zisimamiwe kwa karibu ili kuhakikisha hayo mambo hayatokei,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya wapinzani kuzuiwa kufanya mikutano, Kanali Lubinga alisema: “Mikutano ina taratibu zake, kwa mfano mikutano ya wabunge kwenye majimbo yao na madiwani kwenye maeneo yao haijazuiliwa. Tunapomaliza uchaguzi siasa zinahamia bungeni. Sasa kama kuna mikutano inayoweza kuvuruga amani lazima izuiliwe.”