VIDEO: Dk Bashiru asema CCM haing’oki madarakani kwa mijadala mitandaoni

Katibu Mkuu wa CCM,  Dk Bashiru Ally

Muktasari:

Katibu Mkuu wa CCM,  Dk Bashiru Ally Amesema chama hicho tawala hakiwezi kung’oka madarakani kwa mijadala inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii

Mwanza. Katibu Mkuu wa CCM,  Dk Bashiru Ally Aamesema chama hicho tawala hakiwezi kung’oka madarakani kwa mijadala inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii.

Dk Bashiru ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 22, 2019 katika ziara yake ya kukagua miradi na maendeleo ya chama hicho tawala mkoani Mwanza.

Ametamba kuwa CCM itaendelea kushinda chaguzi na kuongoza dola kwa zaidi ya miaka 100 ijayo kutokana misingi imara iliyonayo na kukubalika kwa wapiga kura.

“Kuing’oa CCM madarakani kunahitaji mkia mrefu. CCM haiwezi kung’oka kupitia mijadala ya kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu kura zinapigwa na wananchi.”

“Sikuhizi nasikia kuna mijadala (kwenye mitandao kuwa) kuna watu wana vipara, wengine wana majipu sijui, lakini kwa misingi ya CCM, binadamu wote ni sawa. (wawe) mwenye kipara na asiye na kipara. Uwe na mkia, usiwe na mkia. Binadamu wote ni sawa,” amesema Bashiru.

Licha ya kutoweka wazi siku za hivi karibuni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe alimtaka  mfanyabishara maarufu, Rostam Aziz kuacha kuzungumzia watu badala yake ajikite kuzungumzia “mambo makubwa ya nchi”.

Alikuwa akijibu swali kuhusu ushauri uliotolewa na Rostam kwake kwamba asichukue fomu za kuomba kupitishwa na CCM kuwania urais mwaka 2020 kama ilivyo utamaduni wa chama hicho tawala.

Katika maelezo yake Membe alisema, “Rostam ni economist (mchumi). Sasa huu ndio ushauri wangu kwake kwamba aji-address, he does better anapoji-address (anafanya vizuri anapozungumzia uchumi) na masuala ya kiuchumi.

“Na asijaribu kuwa christian than Romans (Mkristo kuliko Warumi). Nadhani mtanielewa. Rostam, wewe ni mwenzetu sisi, tumekata mikia, au sio bwana. Ukikata mkia umekata mkia tu. Hata ujitahidije, mkia wako ni mfupi tu.”

Lakini leo Dk Bashiru bila kutaja majina wala kufafanua amesema “Sura yako haituhusu, majipu yako hayatuhusu. Labda kama yanadhuru Serikali tunayatumbua. Kwa hivyo, mijadala rojo rojo ninayoisikia kwenye mitandao, mengine ya wana CCM haituyumbishi”

Kuhusu namna ya kupata viongozi, Dk Bashiru amesema kipindi cha uongozi kupatikana kupitia figusufigisu kimepita kwa sababu CCM inao viongozi wanaoujua mchezo wa siasa, imara, jasiri, shupavu, watiifu kwa umma na wanaoheshimu, kulinda na kufuata katiba ya chama na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuhusu uimara wa CCM iliyopokea uongozi wa dola kutoka vyama vya ukombozi vya Tanu (Tanzania Bara) na Afro Shirazi (ASP) kilichokuwa kinaongoza Tanzania Visiwani, Dk Bashiru ametaja uongozi bora na imara wa Rais John Magufuli ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Taifa, ujenzi wa uchumi imara na kukubalika kwa wananchi kuwa miongoni mwa mitaji ya chama hicho.

“Umoja wetu miongoni mwa wanachama, fikra sahihi ambayo misingi yake ni uhuru, haki na usawa na kukubarika kwa umma ndiyo nguvu inayoifanya CCM isiweze kung’oka madarakani kwa zaidi ya miaka 100 ajayo.”

“Ukiisha linda Uhuru wa nchi, ukalinda rasilimali zisiporwe, ukahakikisha Serikali haiyumbishwi wala kupangiwa cha kufanya na kutofanya na wakubwa (wafadhili/wahisani) na kuwekeza kwenye maisha ya watu.....Serikali hiyo itakubalika kwa umma; tumefanya hivyo kwa muda mrefu,” amesema.

Kuhusu kukosoa, Katibu Mkuu huyo amesema ni wajibu na haki ya wana CCM kusema ukweli na kukosoa na kuonyesha namna ya kusahihisha kosa hilo. Nayekosoa kwa kutumia misamiati isiyoeleweka huyo anaweza akawa mwana CCM nyemelezi.

“Hatuwezi tukasumbuka na watu wenye vinyemelezi au wanachama nyemelezi (kwa) sababu chama hiki ni kikubwa” amesema Dk Bashiru

Amewataka wana CCM kuwa wajasiri kukosoa chama na Serikali kwa lugha ya kiungwana na yenye adabu kulingana na mila na desturi za chama ya kutanguliza kwanza maslahi ya umma.