Dk Bashiru asema Sh50 milioni kila kijiji hazipo

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk  Bashiru Ally

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amezungumzia ahadi ya Sh50 milioni kila kijiji iliyotolewa na chama hicho katika kampeni za uchaguzi mwaka 2015, kubainisha kuwa Serikali haiwezi kugawa fedha hizo nyumba hadi nyumba

Dodoma. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk  Bashiru Ally amezungumzia ahadi ya Sh50 milioni kila kijiji iliyotolewa na chama hicho katika kampeni za uchaguzi mwaka 2015, kubainisha kuwa Serikali haiwezi kugawa fedha hizo nyumba hadi nyumba.

Amesema badala yake chama hicho tawala kitatumia rasilimali fedha kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Mwaka 2015, CCM iliahidi kuwa iwapo ingeshinda Uchaguzi Mkuu, ingetekeleza programu maalumu ya kutoa Sh50 milioni kwa kila kijiji ili fedha hizo zitumike kuchochea maendeleo ya watu wa vijiji hivyo.

Akizungumza leo Jumapili Agosti 4, 2019 katika kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa na televisheni ya Star TV, Dk Bashiru aliyekuwa akizungumzia utekelezaji wa ilani ya CCM, amesema ilani si msahafu.

“Sh50 milioni kila kijiji hazitatoka, wewe unatoka kijiji gani? (alimuuliza mwongoza kipindi). Mtaa wa Sukuma, hatuwezi kupeleka pesa namna hiyo tukakupa wewe tukampa yule. Pesa zile ni mpango uwezeshaji wa kiuchumi,” alisema Dk Bashiru.

Alitaja baadhi ya miradi kuwa ni ule wa umeme vijijini (Rea),  ambao gharama ya kuweka nishati hiyo ni  kati ya Sh300,000 hadi 400,000 lakini wananchi wanachangia Sh27,000 tu.

“Tunasema kwa miaka mitano kwa hadi 2020, wananchi wa pembezoni ya miji na vijijini walipe Sh27,000 tu, tunatafuta namna ya kuwawezesha ili mwananchi masikini auze kuku wake wawili au watatu afunge umeme, akishafunga umeme atajiwezesha kwa namna mbalimbali.”

“Kwa hiyo zile Sh50 milioni labda wakaamua kuchinja ng’ombe na kusherehekea mwaka mpya, zimetolewa katika mtindo wa bajeti ya maendeleo ambayo yatasisimua kasi ya kuleta maendeleo na kujikomboa kiuchumi,” amesema Dk Bashiru.

Alitaja pia fedha za mikopo ya asilimia 10 kwa halmashauri inayotolewa kwa wanawake, vijana na wenye walemavu kuwa miongoni mwa fedha hizo, huku pia akitaja utoaji wa elimu kuwa moja ya matumizi ya fedha hizo.

“Nataka kujenga hoja kwamba tuliahidi kutumia rasilimali za kodi na mikopo ya Serikali na vyanzo vingine kwenye mfuko letu tuwezeshe wananchi wetu.”

“Nina uhakika hakuna mwananchi aliyekuwa anasubiri agawiwe pesa kwa sababu wanajua hakuna Serikali inayogawa pesa nyumba kwa nyumba,” amesema Dk Bashiru.