Dk Bashiru atetea uteuzi wa wabunge waliohamia CCM

Friday April 26 2019

 

By Airea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema uteuzi wa wabunge wanaohama vyama vya upinzani na kupitishwa kugombea tena kupitia CCM huzingatia mwongozo wa chama, sifa pamoja na maamuzi ya kamati kuu.

Hayo ameyasema leo Aprili 26, 2019 akihojiwa na Tido Mhando katika kipindi cha Gumzo la Muungano kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC 2).

Dk Bashiru amesema miongozo ya chama iko bayana juu ya namna ya kumpata mgombea ikiwemo kura za maoni kuhusu uteuzi wa wagombea na kuchujwa huku  akibainisha kuwa kikao cha mwisho cha uteuzi wa uchaguzi mdogo ikiwa ni kamati kuu.

“Ukiangalia katika kura za maoni za uchaguzi mdogo wa Korogwe zilitofautiana na uteuzi wa kamati kuu hiyo ikimaanisha kuwa kura za maoni si chombo cha mwisho bali kamati kuu,” amesema Dk Bashiru.

Amesema kurudi kwa wabunge hao na kukubali kuwa wanachama ndiyo kunawafanya kuwa na sifa ya kuteuliwa tena huku chama kikizingatia uwezo wa waombaji kwa sifa zao na nguvu ya chama chenyewe.

“Hawa watu wanatoka katika upinzani ambako hakuna nguvu wakija kwetu watakuwa na nguvu ya kushinda na kwa sababu walikuwa wabunge tutawarudisha tena katika majimbo yao kwa sababu ndiyo sehemu wanayokubalika,” amesema Dk Bashiru.

Amesema huo ndio utaratibu wa chama kinachotaka kujijenga kwa ushindani na suala hilo lilipata baraka zote.

“Na atokee mtu aseme kuna mtu alitaka kuchukua fomu na akakataliwa atokee, watu 33 na amepatikana mtu mmoja. ”

Advertisement