Dk Bashiru atoa ombi kwa waandishi kuhusu Mwalimu Nyerere

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amekutana na kufanya mazungumzo na wahariri wa vyombo vya habari Tanzania jijini Dodoma, amewaomba kutumia nafasi zao kuandika mambo yaliyofanywa na muasisi wa taifa hilo, Mwalimu Julius Nyerere

Dodoma. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewaomba waandishi wa habari na wahariri wa vyombo vya habari Tanzania kuutumia mwaka 2019 kutangaza mambo aliyofanya Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya kusaidia vijana wa kizazi cha sasa.

Dk Bashiru ameyasema hayo leo Ijumaa Mei 3, 2019 katika mazungumzo yake na wahariri wa vyombo vya habari nchini jijini Dodoma.

Amesema kizazi cha sasa vijana wengi hawajui historia ya Mwalimu Nyerere katika taifa la Tanzania  pamoja na mapambano ya kiongozi huyo katika ukombozi wa nchi zingine.

"Lakini asiandikwe kama makasuku kwa kuwa hakuwa malaika bali alikuwa binadamu kama wengine, kwenye kukosoa akosolewe ingawa yafanyike hayo kwa adabu mkijua alikuwa ni kiongozi wa nchi yetu," amesema Dk Bashiru.

Amemsifia muasisi huyo wa taifa kuwa alifanya kazi ya kupigania haki za kuchagua na kuchaguliwa kwa kila mtu bila kujali chama chake.

Ametumia mfano wa vijana wengi kuwa hawajui historia hata ya bara la Afrika, kwani mwaka 2006 aliwauliza wanafunzi 32 wa mwaka wa pili wa chuo kikuu lakini walishindwa kujua Samora Machel ni nani.

Kuhusu Uhuru wa habari, amesema mapambano ya uhuru ni ya kudumu kwani mahitaji ya watu yanaongezeka kila siku.