Dk Bashiru awaonya Ma RC Mwanza, Morogoro

Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally

Muktasari:

  • Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amemuonya mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na mwenzake wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe, akiwataka kusimamia ipasavyo shughuli za Serikali katika maeneo yao

Bariadi. Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amemuonya mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na mwenzake wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe, akiwataka kusimamia ipasavyo shughuli za Serikali katika maeneo yao.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Agosti 8, 2019 katika kilele cha maonesho ya kitaifa ya Nanenane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

Dk Bashiru ametaja kitendo cha Dk Kebwe kushindwa kumshughulikia mkurugenzi wa halmashauri ambaye hakumtaja,  anayedaiwa kutumia Sh60 milioni zilizotolewa kwa ajili ya matumizi maalum kununulia dawa ya mchwa.

"RC hakushughulika na mkurugenzi huyu hadi Rais (John Magufuli) alipoingilia kati. Kwa Simiyu chini ya uongozi wa Mtaka (mkuu wa Mkoa wa Simiyu-Anthony Mtaka) haya yasingetokea. RC Morogoro pokea ujumbe wangu," amesema.

Dk Bashiru pia ametuma ujumbe kama huo kwa Mongella akimtaka kumsimamia na kumbana mkurugenzi wa halmashauri ya Sengerema (hakumtaja) aliyeshindwa kutaja kiwango cha bajeti ya miundombinu ya barabara.

Huku akimwagia sifa Mtaka kuwa miongoni mwa wakuu wa mikoa wachapa kazi nchini, Dk Bashiru amesema ufanisi wa Serikali unategemea ushirikiano na uwajibikaji miongoni mwa viongozi na watendaji.

Katibu Mkuu huyo pia ametangaza kuondoa kauli yake kuhusu migogoro miongoni mwa viongozi wa CCM na Serikali mkoani Mara aliyosema ilikuwa inakwamisha maendeleo aliyoitoa kwenye kilele cha Nanenane mwaka 2018.

"Nawapongeza viongozi wa Mara kuwa hali sasa iko shwari. Naondoa kauli yangu ya mwaka jana kuhusu mkoa wa Mara," amesema Dk Bashiru huku viongozi wa mkoa wa huo wakijipongeza kwa kupeana mikono.

Katika hotuba yake mwaka jana, Dk Bashiru alitaja mikoa ya Mara, Arusha na Dar es Salaam kuwa miongoni mwa inayoongoza kwa migogoro miongoni mwa viongozi aliyosema inakwamisha utekelezaji wa ilani ya CCM huku akiwaagiza viongozi wa mikoa hiyo kujirekebisha.