Dk Bashiru awaonya wanasiasa waropokaji

Katibu wa CCM Taifa Dk Bashiru Ally, akipokelewa na kijana wa Chipukizi,mara baada ya kuwasili eneo la Kia,Mkoani Kilimanjaro. Picha na Florah Temba

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amewaonya wanasiasa nchini Tanzania kuachana na tabia ya kuropoka maneno yanayoweza kuhatarisha usalama wa Taifa

Siha. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amewaonya wanasiasa nchini Tanzania kuachana na tabia ya kuropoka maneno yanayoweza kuhatarisha usalama wa Taifa.

Ametoa kauli hiyo jana Jumapili Julai 7, 2019 katika kikao cha ndani kilichofanyika Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro na kuwahusisha viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho tawala nchini Tanzania.

Dk Bashiru aliyepo mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya siku nne amesema wanasiasa wakianza kuropoka nchi itapotea.

“Mtu akiropoka mnamjibu palepale ili kutuliza hali ya hewa kwa sababu waropokaji hawapo Kenya peke yake na Tanzania wapo,” amesema Dk Bashiru akitolea mfano kauli isiyofaa iliyotolewa hivi karibuni na mwanasiasa mmoja nchini Kenya.

Alitumia nafasi hiyo kuwataka viongozi wa chama na Serikali kuwa makini na taarifa za upotoshaji, kutoamini kila taarifa wanayoiona mitandaoni.