Dk Bashiru awataka viongozi Manyara kujenga ofisi ya CCM

Friday July 12 2019

Katibu Mkuu wa CCM Dk Bashiru Ally akizungumza

Katibu Mkuu wa CCM Dk Bashiru Ally akizungumza kwenye mkutano wa ndani wa viongozi wa matawi, kata na wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara leo. Picha na Joseph Lyimo 

By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Kiteto. Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amewaagiza viongozi wa chama hicho Mkoa wa Manyara kujenga ofisi mpya yenye hadhi.

Amesema chama hicho tawala kinatakiwa kuwa na ofisi ya kisasa si kama ofisi za vyama vingine vya siasa.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Julai 12, 2019 wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara akibainisha kuwa ofisi iliyokuwepo ilichomwa moto.

"Baadhi ya viongozi walifanya ubadhirifu na kuichoma ofisi moto ila hayo ni ya miaka iliyopita jengeni ofisi msiwe kama vyama vingine vya siasa havina ofisi ila vipo katika mitandao," amesema Bashiru.

Amesema hali ya uchumi wa mkoa huo ni nzuri hivyo wanapaswa kujipanga na kuwa na ofisi ya kisasa yenye kukidhi vigezo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Simon Lulu amemhakikishia Dk Bashiru kuwa wanajipanga kutekeleza agizo hilo.

Advertisement

"Tumezungumza na wanachama wetu wa kawaida, viongozi wakiwemo madiwani, wabunge, wakuu wa wilaya na mkuu wa mkoa watuchangie kwenye ujenzi huo," amesema Lulu.

CCM Manyara yatakiwa kujenga ofisi ya kisasa inayoendana na hadhi yake

Advertisement