KAKAKUONA: Dk Bashiru ni kama anapiga ngoma katika maji

Wiki iliyopita, Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alitoa kauli iliyowapa faraja wapenda demokrasia pale alipowataka polisi kutotumia mabavu kushughulikia migogoro ya kisiasa.

Bahati mbaya sana, kauli ya Dk Bashiru ambaye ni mmoja wa viongozi wa juu wa chama kinachotawala, inaelekea imewaingia polisi kupitia sikio moja na kutokea sikio la pili.

Nasema hivyo kwa sababu baada ya kuitoa Ijumaa iliyopita, haikuchukua muda tukashuhudia polisi wakiendeleza ubabe dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani katika mikutano yao ya ndani.

Mfano wa karibuni kabisa ni hatua ya Jeshi la Polisi kusambaratisha mikutano ya ndani wa mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee huko Bariadi na Bukoba.

Dk Bashiru katika kauli yake alisema “Tukianza kutumia mabavu katika kutatua migogoro yetu (ya kisiasa) ni dalili za kushindwa kuongoza nchi, kwani hakuna sababu wakati wananchi wanatii sheria.”

Kwa muda sasa kumekuwapo na wimbi la polisi kuwakamata viongozi wa kitaifa na wabunge wa vyama vya upinzani, ama kwa madai ya mikusanyiko isiyo halali au kufanya mikutano ya ndani bila kibali, jambo ambalo halisikiki kwa mikutano ya CCM.

Hatua hii ya jeshi letu la polisi inafikirisha sana, hasa inapoonekana ni kosa kwa viongozi wa upinzani kufanya mikutano ya ndani lakini matendo hayohayo yakifanywa na viongozi wa CCM huwa ni halali.

Ni lazima tujitafakari kama taifa, ni mbegu ya aina gani tunaipandikiza katika taifa linalojipambanua kuheshimu misingi ya utawala bora inayoheshimu utawala wa sheria ikiwamo kuheshimu katiba.

Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 imeeleza kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Ibara hiyo inaongezewa nguvu na kanuni za maadili ya vyama vya siasa za mwaka 2007, kama zilivyotangazwa katika gazeti la Serikali (GN) namba 2015 ya Oktoba 12 mwaka 2007.

Kubwa zaidi katika kanuni hizo ni kifungu cha 4(1) (e) ambacho kimesisitiza kuwa chama cha siasa kitakuwa na haki ya kufanya mikutano kisiasa na maandamano kwa mujibu wa Katiba na sheria.

Ni dhana iliyo wazi kwamba kundi moja linapojihisi linakandamizwa na watawala kwa sababu za kisiasa, litatafuta njia ya kujitetea.

Kauli ya Dk Bashiru, haitofautiani sana kimaudhui na kauli ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres akiwa Nairobi nchini wiki iliyopita, akionya juu ya viini vya ugaidi Afrika.

Katibu mkuu huyo wa UN alisema ugaidi hauwezi kuibuka tu kutoka hewani, bali ni pale ambapo haki za binadamu zinakiukwa, utawala bora unapuuzwa na matarajio yanafifishwa na kundi mojawapo.

Kama tumekubali taifa letu linaendeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, basi tuishi na kutenda kama mfumo unavyotaka na vyama vyote viruhusiwe kucheza mpira kwenye uwanja wa ukoka.

Tukipendelea timu fulani icheze kwenye ukoka na nyingine icheze uwanja wenye mawe na mbigiri, nawaambia huo ubaguzi kamwe hautatuacha salama. Tusije kumbuka shuka wakati kumekucha.