Dk Kigwangalla ampoza Makamba mtandaoni

Muktasari:

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amempoza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba kuhusu mradi wa kupandisha watalii katika Mlima Kilimanjaro kwa kutumia viberenge (cable cars), akitamka kuwa “yamekwisha.” 

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amempoza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba kuhusu mradi wa kupandisha watalii katika Mlima Kilimanjaro kwa kutumia viberenge (cable cars), akitamka kuwa “yamekwisha.”

Jana Jumapili Julai 7, 2019 baada ya akaunti ya Twitter ya Haki Ngowi kuweka taarifa kuwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) inatarajia kuanzisha usafiri wa kutumia magari ya umeme yanayopita juu ya nyaya kupeleka watalii kwenye mlima huo, mawaziri hao walipishana kauli.

Baada ya andiko hilo, Makamba alijibu, “Itabidi watu wetu wa mazingira tupitishe na kutoa cheti kwanza kabla hawajaanza na tutafanya tathmini ili kujua matokeo kwa mazingira na mkakati wa kudhibiti.”

Maelezo hayo ya Makamba yalijibiwa na Dk Kigwangalla ambaye aliandika, “Hivi kuna nchi ngapi zimeweka cable cars kwenye milima yake? Hizi haziharibu mazingira. Cable car inapita juu inaharibu mazingira gani?”

“Zaidi ya ekari 350,000 za misitu zinapotea kila mwaka nchini. Ipi risk (janga) kubwa? Watu wa mazingira wamechukua hatua gani zaidi ya makongamano.”

Lakini leo Jumatatu Julai 8, 2019 katika akaunti ya Twitter, Dk Kigwangalla ameandika, “It’s a beautiful Monday (Ni Jumatatu nyingine nzuri) tunaanza upya. Mtani wangu (Makamba) anajua wazi kuwa kila mradi tunaoufanya lazima ufanyiwe EIA (Tathmini ya athari ya mazingira).”

“Hakukuwa na haja ya kuleta twitani jambo lile, lakini yameisha. Tumesameheana kwa yote, Wakimbu wangu walikaa vibaya jana  nilioverreact.”

Kwa upande wake, Makamba ameandika, “Ndugu yangu, naomba hili jambo liishe. Tunajenga nyumba moja ya Watanzania. Hii ni kazi ya umma leo upo kesho haupo, tulipoghafirika tusameheane na sasa tutazame mpira #AFCON2019.”