Dk Kijaji agoma kukagua ukarabati Shule ya Pugu

Muktasari:

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji jana Jumanne alishindwa kuendelea na ukaguzi wa ukarabati wa Shule ya Sekondari Pugu, Dar es Salaam baada ya viongozi mbalimbali wa manispaa ya Ilala kutokuwa na taarifa za ukaguzi wake

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji amelazimika kuahirisha kukagua ukarabati wa shule kongwe ya Sekondari ya Pugu jijini Dar es Salaam baada ya uongozi wa mkoa na manispaa ya Ilala kueleza hawajui lolote kuhusu ukarabati huo.

Dk Kijaji alichukua uamuzi huo jana Jumanne Februari 19, 2019 baada ya kaimu katibu tawala mkoa wa Dar es Salaam, Yokobeth Malisa, ofisa mipango manispaa ya Ilala, Ando Mwankuga, ofisa elimu taaluma mkoa na mkuu wa shule, Jovinus Mutabuzi wote kwa pamoja, kuukana mradi huo.

Mradi huo unaogharimu Sh1 bilioni unatekelezwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) chini ya ukandarasi wa Shirika la Nyumba Tanzania NHC, lakini mkataba wake pamoja na mpango wa kazi inayotakiwa kufanyika haijulikani kwa viongozi wa halmashauri.

"Mradi huu una changamoto kubwa, hatujawahi kuona mkataba wake kuanzia mkoani hadi manispaa ya Ilala pamoja na uongozi wa shule, kwa hiyo hatujui umegharimu kiasi gani na ni vitu gani viko kwenye mkataba huo jambo linalotuwia vigumu kuuelezea," alisema Ando Mwankuga.

Mwankuga alisema yeye ndiye mwenye taarifa ya miradi yote inayotekelezwa katika ngazi ya manispaa ambayo kwa mujibu wa taratibu na kanuni hupitishwa kwenye vikao mbalimbali ikiwemo kamati ya ushauri ya manispaa na Baraza la Madiwani, na kwamba mradi huo wa ukarabati wa shule ya Sekondari Pugu haujawahi kujadiliwa

Kwa upande wake, mkuu wa shule hiyo, Mutabuzi alisema taarifa alizonazo ni za kuambiwa kwamba mradi huo umegharimu zaidi ya Sh900 milioni, lakini hajawahi kushirikishwa kikamilifu kuhusu ukarabati huo na yeye amekuwa akiwaona mafundi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa wakiingia kufanya kazi na kutoka shuleni hapo.

"Mimi naona tatizo kubwa hapa ni mawasiliano hafifu kati ya wizara ya elimu na halmashauri manispaa ya Ilala, ndio maana haya yote yamejitokeza" alisema Mutabuzi

Kaimu katibu tawala wa mkoa aliahidi kupeleka taarifa kwa katibu tawala wa mkoa huo ili aitishe vikao vya wadau wanaohusika ili kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.

Alieleza yeye binafsi akiwa miongoni mwa wasimamizi wa masuala ya miradi ya maendeleo ya mkoa hakuwa na taarifa ya uwepo wa mradi huo na haujawahi kuripotiwa mahali popote kwenye vikao.

Dk Kijaji alishangazwa kwa kuona mradi kama huo wenye thamani kubwa, utaratibu wake wa ushirikishanaji miongoni mwa wadau wanaohusika haujakaa vizuri hivyo akaamua kusitisha ukaguzi wake.

"Kama hali ndiyo iko hivi, mmeukana mradi huu kwamba hamuujui, sasa mimi nitakagua nini? Tuondoke!" alielezea kwa masikitiko Dk Kijaji na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo.