Dk Kimei awaaga wanahisa CRDB ikiwaongezea gawio

Muktasari:

Kwenye mkutano mkuu uliofanyika Mei mwaka jana jijini Arusha, Dk Kimei alitangaza nia yake ya kustaafu baada ya kuiongoza benki hiyo kwa zaidi ya miaka 20 .

Ingawa wengi walionyesha mashaka ulipotangazwa mpango wa aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei kustaafu, hofu yao imeondoka baada ya kuona taasisi hiyo inazidi kuimarika.

Kwenye mkutano mkuu uliofanyika Mei mwaka jana jijini Arusha, Dk Kimei alitangaza nia yake ya kustaafu baada ya kuiongoza benki hiyo kwa zaidi ya miaka 20 kitendo kilichowainua baadhi ya wanahisa na kusema uamuzi huo uahirishwe kwani sekta ya benki ilikuwa inapitia kipindi kigumu hivyo CRDB bado inamhitaji.

Pamoja na maombi hayo, Oktoba mwaka jana, benki hiyo ilimtambulisha mkurugenzi mpya, Abdulmajid Nsekela ambaye kwa kipindi kifupi alichohudumu, amefanikiwa kupandisha gawio la wanahisa kutoka Sh5 walizopokea mwaka jana hadi Sh8 mwaka huu kwa kila hisa moja likiwa ni ongezeko la asilimia 60.

Kutokana na hali hiyo, nyoyo za wengi zimetulia na wakapendekeza Dk Kimei aagwe kwa heshima kwani mchango wake ulikuwa mkubwa ndani ya taasisi hiyo. Mwaka mmoja baadaye, Dk Kimei amewaaga wanahisa na menejimenti ya benki hiyo kwa utulivu.

“Nimekuwa mkurugenzi mtendaji wa benki hii kwa miaka 22. Kwa nafasi niliyokuwa nayo, nilikuwa nafanya uamuzi. Huenda katika utekelezaji wa majukumu yangu kuna niliyemkwaza kwa namna moja au nyingine. Naomba anisamehe. Kama mzazi aliyemlea mtoto wa miaka 22, nina mapenzi makubwa na Benki ya CRDB na nitamsaidia mkurugenzi mpya wakati wowote atakapohitaji mchango wangu,” amesema Dk Kimei.

Kimei amesema anamfahamu Abdulmajid kwa muda mrefu sasa na kwamba anazo sifa na vigezo muhimu vinavyohitajika kuiongoza benki hiyo ila akabainisha kuwa anahitaji ushirikiano kufanikisha malengo yaliyopo.

Hofu ya wanahisa wengi iliyojitokeza kwenye mkutano mkuu wa 23 wa benki hiyo ilikuwa ni uwezekano wa kufanya vibaya endapo Dk Kimei angeondoka. Katika kipindi hicho, faida ya benki nyingi ilishuka na uwiano wa mikopo isiyolipika ulikuwa mkubwa.

Lakini baada ya mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, Ally Laay kuwaeleza kuwa faida ya mwaka 2018 imeongezeka kutoka Sh36.2 bilioni iliyopatikana mwaka 2017 hadi Sh64.1 bilioni mwaka jana hivyo kupandisha gawio la kila hisa kwa asilimia 60, waliamini wapo kwenye mikono salama.

Laay anasema CRDB ni benki ya kizalendo inayomilikiwa na Watanzania kwa zaidi ya asilimia 90. “Watanzania wa kawaida zaidi ya 29,000 wanamiliki zaidi ya asilimia 43 ya hisa za CRDB,” anasema Laay.

Licha ya ongezeko la faida, taarifa za fedha za benki hiyo zinaonyesha uwiano wa mikopo isiyolipika umepungua kutoka asilimia 11.9 iliyokuwepo mwaka 2017 hadi asilimia 10.4 mwaka 2018.

Laay amesema faida ya sekta nzima ya benki imeongezeka na kufika Sh273.2 bilioni mwaka 2018 kutoka Sh208.9 bilioni iliyopatikana mwaka 2017.

“Nilikuwa miongoni mwa waliokuwa na hofu juu ya kustaafu kwa Dk Kimei lakini sasa sina kwa kuwa kijana aliyelelewa na mzee wetu ndiye alirithi mikoba,” anasema kampteni mstaafu, Nkoswe Noel, mwanahisa wa benki hiyo kutoka Sumbawanga.

Mwanahisa mwingine, Dk Davis Mabeba anasema: “Mwaka jana kulikuwana sintofahamu, tulidhani benki ingefanya vibaya akiondoka Kimei kumbe sio. Tunaipongeza menejimenti kwa hatua hii.”

Akipokea Baraka za Dk Kimei, mkurugenzi mpya, Nsekela amesema benki itaendelea kushirikiana vyema na wadau wote kuhakikisha inakidhi matarajio ya kila mmoja.

Kutoa mfano wa anachokisema, aliyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Bunge lililompongeza ofisa anayehudumu kwenye tawi la benki hiyo lililopo kwenye viunga vya mhimili huo.

“Tunapoona mtu au taasisi anapongeza huduma zetu, tunachukua hatua. Hivi karibuni, wabunge na spika walipongeza huduma wanazopata kupitia tawi letu lililopo kwenye viunga vya Bunge na wakamtaja Grace Adam kutokana na kazi nzuri anayoifanya. Nasi tumeliona hilo na tumempandisha cheo,” alisema Nsekela kwenye mkutano wa wanahisa.

Serikali pia imeahidi kuendelea kushirikian vyema benki hiyo kwa siku zijazo ili kujenga uchumi imara wa Taifa. Akizungumza kwenye semina waliyoandaliwa wanahisa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema CRDB ni benki inayojali uwajibikaji hivyo mchango wake kwenye uchumi ni muhimu.

“Serikali inaitazama CRDB kama benki ya kimkakati,” amesema Majaliwa.