Dk Ndugulile: Wafundisheni wananchi umuhimu wa kuacha wosia

Muktasari:

  • Wosia unaochwa na mume una nguvu katika kuepusha manyanyaso ya ndugu kwa mjane na husaidia kuepusha kudhurumiwa mali alizochuma na kumiliki pamoja na mumewe

Dodoma.  Watendaji wote wa Serikali wameagizwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuandika wosia kabla hawajafa ili kuondoa migongano na manyanyaso kwa wajane, yanayotokana na kugombania mali za marehemu.

Wito huo umetolewa leo Jumapili Juni 23, 2018 na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya wajane Duniani, yaliyofanyika Kitaifa Jijini Dodoma.

Dk Ndugulile amesema kumekuwa na malalamiko mengi na manyanyaso kutoka kwa wajane ambao wamekuwa wakidhulumiwa mali pindi waume zao wanapofariki na kuwaacha na watoto.

“Elimu inatakiwa kutolewa kwa wananchi wote kuhusu umuhimu wa kuacha wosia ili wakati mjane anapomlilia mwezake siyo ndugu waanze kupora

hati za nyumba, mali na kumwacha mama mjane akiwa hana kitu na wengine hufika mbali zaidi na kuwafukuza hata kwenye nyumba walizokuwa wanaishi,” amesema Dk Ndugulile.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la wajane Tanzania (Tawia), Rose Sarwati amesema wajane wengi wamekuwa wakidhulumiwa haki zao ikiwemo ya kumiliki ardhi hata waliyokuwa wakiimiliki na waume zao.

“wengine wamekuwa wakihusishwa na tuhuma za mauaji ya waume zao kwa kudhaniwa kuwa ni wachawi na hivyo kufukuzwa au kuuawa kabisa ili wasirithi mali.”

Naye Katibu Mkuu Wa Wizara ya Afya, Idara ya maendeleo ya jamii Dk John Jingu amesema idadi ya wajane ulimwenguni kote ni 258 milion kuhu Tanzania ikiwa na wajane 800,000 sawa na asilimia 3 ya wanawake wote nchini.