Dk Ndugulile aeleze jinsi madaktari Hospitali ya Iringa wanavyohudumiwa

Wednesday June 26 2019

 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Katika mwaka wa fedha 2018/19 Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa ilitenga Sh40 milioni kwa ajili ya kuwalipia gharama za nyumba madaktari wao ambapo hadi Mei 2019 kiasi cha Sh25.5 zilishatolewa.

Akijibu swali bungeni leo Jumatano Juni 26,2019 Naibu Waziri wa Afya Dk Faustin Ndugulile amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kutolea huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya motisha kwa watumishi.

Naibu waziri huyo alikuwa anajibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Ritha Kabati ambaye ameuliza ni mkakati gani Serikali imeweka katika kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba kwa ajili ya madaktari bingwa jambo linalosababisha madaktari kuishi mbali.

Kuhusu upungufu wa watumishi, Dk Ndugulile amesema mwaka 2018 Serikali ilisomesha madaktari 100 na mwaka huu inasomesha zaidi ya madaktari wengine 100 ambao watapangwa katika maeneo yenye uhitaji.

Advertisement