Dk Possi ampa mtihani Lissu

Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi amemtaka mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kutoa ushirikiano kwa Polisi kusaidia uchunguzi wa shambulio lake la risasi na watu wasiojulikana.

Dk Possi aliyekuwa akijibu madai ya Lissu aliyoyatoa hivi karibuni nchini humo alipohojiwa katika kipindi cha News Africa cha kituo cha televisheni cha Deutsche Welle (DW), alisema uchunguzi wa tukio hilo ulianza baada ya kutokea Septemba 7, 2017, Dodoma.

Tangu aliposhambuliwa na hatimaye kusafirishwa kwenda Nairobi, Kenya na baadaye Brussels nchini Ubelgiji kutibiwa, Lissu amekuwa akiituhumu Serikali kuhusika na shambulio hilo na kwamba tangu wakati huo Polisi haijakamata mshukiwa yeyote.

Hivi karibuni Lissu amekuwa akifanya mahojiano na vyombo vya habari vya kimataifa, alianza na BBC World ya Uingereza baadaye DW ya Ujerumani na anatarajia kwenda Marekani.

Akijibu madai ya Lissu aliyoyatoa Ujerumani, Dk Possi alisema Serikali imekuwa ikilifuatilia suala hilo ikiwamo kuanza uchunguzi.

Dk Possi alisema Serikali inafuatilia suala hilo ndiyo maana Rais John Magufuli alishatoa tamko kulaani tukio hilo na kutuma baadhi ya viongozi kumjulia hali jijini Nairobi.

“Rais alitoa taarifa ya kulaani tukio hilo na kuagiza uchunguzi wa kina wa haraka. Kwa nyakati tofauti Rais amemtuma makamu wake, Rais mstaafu na viongozi wengine wa Serikali kumtembelea Lissu akiwa hospitali akiwa Dodoma, Nairobi na Brussels,” alisema Dk Possi katika tamko lake.

Aliongeza kuwa uchunguzi ulishaanza mara tu baada ya kutokea tukio hilo lakini umeshindwa kuendelea kwa sababu ya kutopata ushirikiano kutoka kwa mbunge huyo.

Kuhusu malalamiko ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwa gerezani, Dk Possi alisema hajafungwa bali utaratibu wa kutoa dhamana ni wa kimahakama na unasimamiwa na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

“Kwenye nchi yoyote ya demokrasia ya vyama vingi, kuendelea au vinginevyo kwa vyama vya siasa kunategemea jinsi vilivyojipanga kuuza itikadi zao,” alisema.