Dk Shein apata mpinzani wa urais Zanzibar

Saturday October 18 2014Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein 

By Mwinyi Sadallah, Mwananchi

Zanzibar. Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein, amepata mpinzani iwapo ataamua tena kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao mwakani, baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Tadea, Juma Ali Khatib (50), kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo visiwani humu.

Mgombea huyo ni watatu kujitokeza hadharani na kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo, baada ya katibu mkuu wa CUF, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kutangaza nia hiyo akifuatiwa na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed aliyetangaza pia nia hiyo.

Hamad Rashid alitangaza nia na kusema kuwa atawania nafasi hiyo kupitia CUF, mgombea binafsi au kwa tiketi Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC).

Ikiwa Maalim Seif atawania tena nafasi hiyo, itakuwa ni mara ya tano tangu mwaka 1995, ulipoanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi ulifanyika mwaka 1995, ambapo Seif alishindwa kwa mara ya kwanza na Dk Salmin Amour Juma wa CCM huku mara mbili akichuana na Dk Amani Karume na kushindwa pia.

Katika maelezo yake kuhusu hatua hiyo, Khatib alisema amechukua uamuzi huo kutokana na matatizo yanayowakabili wananchi wa Zanzibar.

“Matatizo ya Wazanzibar ndiyo yaliyonisukuma kuchukua fomu ya urais wa Zanzibar. Huduma za jamii zimezorota, kuongezeka kundi la vijana wasio na ajira mitaani, wazee kuishi mazingira magumu na ongezeko la ombaomba visiwani Zanzibar,”alisema.

Alisema pamoja na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kuundwa Zanzibar miaka minne iliyopita, utendaji wa Serikali katika kuutumikia umma hauonekani.

“Rais anahitaji kuangalia upya viongozi na watendaji aliowateua na kuwapa majukumu. Nafikiri wameshindwa kubuni mipango ya kuwatumikia watu. Utendaji wa watu wanaomsaidia haujengi taswira halisi, baadhi yao wameshindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo,” alisema Khatib.

Alisema pamoja na kuwepo sheria nzuri, kumekosekana utashi na usimamizi makini, juhudi na dhamira ya wazi na kutokuwepo utendaji unaotarajiwa.

Advertisement