Dk Tulia amzuia Heche kujadili mradi wa Stiegler's Gorge

Muktasari:

  • Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amemtaka mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), kusitisha mjadala kuhusu mradi wa kufua umeme Bonde la Mto Rufiji, Stiegler's Gorge hadi hapo Serikali itakapoleta mkataba wa ujenzi wa mradi huo.

Dodoma. Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amemtaka mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche kusitisha mjadala kuhusu mradi wa kufua umeme wa Bonde la Mto Rufiji, Stiegler's Gorge hadi hapo Serikali itakapoleta mkataba walioingia na mhandisi wa ujenzi wa mradi huo.

Naibu Spika ametoa kauli hiyo leo Jumatano Februari 6, 2019 wakati wabunge wakichangia taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini.

Heche amesema kuna watu wamekuwa wakiimba kama kasuku kuhusu mradi huo bila kujua umeme wake utawaka mwaka 2027

Kauli hiyo ilimfanya mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM),  Ally Keisy kuomba kuhusu utaratibu na kumtaka Heche kufuta kauli yake kwa sababu hakuna kasuku bungeni, jambo ambalo Heche alilikubali.

Akiendelea kuchangia, Heche amesema Serikali imetenga Sh700 bilioni katika bajeti yake lakini fedha zilizokwenda ni Sh26 bilioni tu.

Amesema ili kukamilisha ujenzi wa bwawa hilo zinahitajika Sh7.1trilioni na kwamba inahitajika miaka 10 ili kukamilika.

“Arab contractors  inahusika kujenga nyumba na haijawahi kujenga bwawa kokote duniani na imeamua kusub contract kwa kutafuta kampuni nyingine kuipa asilimia 80,” amesema.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alisimama kwa kutumia kanuni ya  64 (1) na kusema Heche amevunja kanuni hiyo kwa kusema uongo bungeni.

Subira amesema Heche alisema uongo kuwa kampuni ya Arab imetafuta mbia lakini ukweli ni kwamba kampuni hiyo ilikuja kwenye zabuni kwa ushirikiano.

Amesema hadi sasa hajatoa asilimia 80 ya kazi alizopewa na kwamba wanamkabidhi kazi mkandarasi huyo.

Subira alimtaka Heche kufuta kauli yake hiyo jambo ambalo lilimfanya mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe kuomba kuthibitisha badala ya Heche.

Hata hivyo, Dk Tulia alimtaka Heche kufuta kauli yake ya kwamba kampuni hiyo imetafuta mbia ambaye itampa asilimia 80 ya kazi hiyo.

Akijibu hoja hiyo, Heche amemtaka kutafuta kumbukumbu rasmi za Bunge ili kuona alichokisema.

“Nimesema kampuni ya Arab haina uwezo wa kujenga mabwawa, sitatoa neno langu.  Kampuni inatafuta masub- contract kujenga bwawa hili. Siondoi maneno yangu,” amesema Heche.

Kauli hiyo ilimfanya Dk Tulia kutoa uamuzi kwa kumtaka Mgalu kuleta mkataba bungeni huku Heche akitakiwa kuthibitisha ukweli wa maneno yake mara utakapofika mkataba huo.

Pia amemtaka kutoendelea na mjadala huo tena hadi suala hilo  litakapomalizwa.