Dk Tulia awakana wabunge walioshiriki semina ya NGO

Monday June 24 2019

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson akizungumza

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson akizungumza bungeni jijini Dodoma leo, alipokuwa akieleza kuwa Bunge halina taarifa ya mkutano wa taasisi zisizo za kiserikali (NGO) na wabunge 40  kwa ajili ya kupewa uelewa kuhusu muswada namba tatu wa marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2019. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amesema Bunge la Tanzania halina taarifa ya mkutano wa taasisi zisizo za kiserikali (NGO) uliowahusisha wabunge 40  kwa ajili ya kupewa uelewa kuhusu muswada namba tatu wa marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2019 uliowasilishwa bungeni na Serikali ya Tanzania.

Dk Tulia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Juni 24, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu mwongozo wa mbunge wa Viti maalum (Chadema), Salome Makamba aliyedai baadhi ya magazeti yameandika habari kuwa wabunge takribani 40 wameshiriki mkutano huo na wamepewa rushwa ili utakapotua bungeni kwa ajili ya kujadiliwa, upitishwe bila vikwazo.

Muswada huo unapendekeza marekebisho katika sheria nane ambazo ni; Sheria ya Makampuni, (Sura ya 212), Sheria ya Hakimiliki (Sura ya 218), Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza (Sura ya 230), Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali (Sura ya 56), Sheria ya Vyama vya Kijamii (Sura ya 337), Sheria ya Takwimu (Sura ya 351),

Sheria ya Uwakala wa Meli (Sura ya 415) na Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini (Sura ya 318).

Kwa mujibu wa Serikali ya Tanzania, mapendekezo ya marekebisho hayo yanalenga kuondoa upungufu uliojitokeza katika sheria hizo wakati wa utekelezaji wa baadhi ya masharti katika sheria husika, na taasisi hizo zimeulalamikia kuwa si rafiki na Jumamosi Juni 22, 2019, zilizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma kutoa malalamiko hayo na pia kukutana na wabunge.

Akitumia kanuni ya 51 (iv) ya Bunge, Salome amesema jana Jumapili Juni 23, 2019 ulifanyika mkutano huo na baadhi ya magazeti yameandika habari kuwa wabunge wamepewa fedha kupitisha marekebisho ya sheria hizo mbalimbali.

Advertisement

“Magazeti na mitandao ya kijamii kunazunguka habari kuwa wabunge wamepewa fedha ili kupitisha muswada huo. Jambo hili limekuwa likitokea mara kwa mara. Naomba busara ya kiti chako,  Bunge liweze kuyawajibisha  kupitia kamati yetu ya maadili ili kuwa fundisho wa magazeti na vyombo vingine vya habari kulidhalilisha Bunge,” amesema Salome.

Akijibu mwongozo huo, Dk Tulia amesema, “Ofisi ya Bunge haina taarifa ya jambo hilo lazima mfahamu namna kamati za Bunge zinavyofanya kazi. Zinafanya kazi kwa maandishi, hakuna mtu anayeruhusiwa kuitisha semina. Labda nje ya hapa na pia awe hajaihusisha ofisi wala haongei mambo ya ofisi.”

“Ukiitisha watu huku kwingine ni mkutano si unaohusu Bunge, kwa hiyo hakuna kibali cha Spika cha kuitisha mkutano uliofanyika jana na mimi namsikia yeye (mbunge), na ofisi mimi niko hapa hatuna hiyo taarifa ya kuita mtu yeyote ya kuja kutoa uelewa kuhusu suala hilo, kwa hiyo kama kilikuwepo ama kilikuwa vipi, chochote kilichoongelewa huko ofisi haina taarifa.”

Advertisement