EU kutobadilika msimamo kuhusu Brexit

Saturday May 25 2019

Umoja wa Ulaya (EU) umesema kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May hakutabadili chochote kwenye msimamo wake kuelekea makubaliano yaliyofikiwa kuiwezesha Uingereza kujiondoa.

Msemaji wa Rais wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Junker amesema ameupokea uamuzi wa May bila furaha na kuongeza kuwa baraza la Uongozi wa Umoja wa Ulaya lilikwishaweka msimamo wake kuhusu makubaliano ya Brexit.

May alitangaza kujiuzulu jana wadhifa wa waziri mkuu baada ya kushindwa kuwashawishi wabunge kuunga mkono mpango wake wa kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit.

Kiongozi wa ujumbe wa majadiliano ya Brexit wa EU, Michel Barnier, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akiusifu msimamo wa May kama waziri mkuu, kwa kufanya kazi kuwezesha Uingereza kuondoka salama kutoka Umoja wa Ulaya.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa wamemsifu May kwa kazi kubwa na ya kujitolea, aliyoifanya kujaribu kukamilisha mchakato wa Brexit kwa maslahi ya nchi yake.

 

Advertisement

 

Advertisement