Ebola yaua wawili nchini Uganda

Thursday June 13 2019

 

Kampala, Uganda. Watu wawili wa familia moja nchini Uganda akiwamo mtoto wa miaka mitano wamefariki dunia kwa ugonjwa wa ebola.

Imeelezwa kuwa mtoto huyo wa kiume alisafiri na familia yake na kuvuka mpaka kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) siku ya Jumapili.

Baada ya hapo alipelekwa katika hospitali moja ya Uganda baada ya kuonyesha dalili ya ugonjwa huo ikiwamo kutapika damu. Taasisi ya Kupambana na Virusi Uganda (UVRI) imethibitisha kuwa vifo hivyo vimetokana na ugonjwa wa ebola.

Wizara ya Afya nchini Uganda ilimtaja mwingine aliyepoteza maisha kuwa ni mwanamke mwenye miaka 50 ambaye ni bibi wa mtoto huyo.

Aidha, watu tisa wameripotiwa kuugua ugonjwa huo hivyo kuwekwa chini ya uangalizi maalumu kuzuia wasiwaambukize wengine.

Tayari wizara ya hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) imetuma kikosi maalumu kutambua wengine walio katika hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo.

Advertisement

Waziri wa Afya wa Uganda, Jane Ruth Aceng amesema familia ya mtoto huyo imeweka katika karantini maalumu kutokana na wengi kuonyesha kuwa na dalili za ugonjwa huo.

Waziri huyo ameliambia gazeti la Daily Monitor la nchini humo kuwa mwanamke huyo ambaye ni Mkongo aliyeolewa Uganda hivi karibuni, aliambatana na watoto wake wanne kwenda kwao kumhudumia baba yake aliyekuwa akiugua ebola.

WHO limethibitisha kuripotiwa kwa ugonjwa huo. Kutokana na tukio hilo, wahudumu 4,700 nchini humo wamepewa chanjo maalum dhidi ya ugonjwa huo.

Advertisement