Elimu ya kilimo yasaidia uvunaji wa pareto iliyo katika ubora

Muktasari:

Pareto ambayo ilianza kulimwa nchini mwaka 1931, hutumika kutengenezea dawa mbalimbali za kuua wadudu, kampuni nyingi za kutengeneza dawa duniani hutumia sumu ya pareto katika kutengeneza bidhaa zao.

Mkulima wa pareto katika Kijiji cha Lwanda, Wilaya ya Mbeya ana kila sababu ya kucheka Januari hii baada kuuza maua yenye sumu kali ya kiwango cha 1.97.

Maua hayo ya pareto hutumika kutengenezea dawa mbalimbali za kuua wadudu.

Lamson Landa ndiye ameibuka kuwa mkulima bora wa zao hilo kwa msimu wa mwaka 2018 katika mikoa ya Mbeya na Songwe.

Mkulima huyo aliuza maua yake kwa Sh3,300 kwa kilo moja, lakini wakulima wengine waliuza kwa Sh2,300 kwa kilo, kutokana na maua yao kutokuwa na sumu ya kiwango kikubwa.

Kiwango cha juu zaidi cha sumu ya maua hayo ni 2.0.

Landa anasema alianza kujihusisha na kilimo cha pareto mwaka 2011 baada kushawishiwa na majirani zake waliokuwa wakilima zao hilo tangu mwaka 2005.

“Sikuwahi kufikiria kujihusisha na kilimo cha pareto, ila nilianza kulima baada ya kushawishiwa na jirani zangu ambao walinieleza kuwa naweza kupata mafanikio makubwa. Tangu nimeanza kulima mafanikio nimeyaona,” anasema Landa.

Alipoanza kilimo hicho, anasema alikuwa anazingatia elimu inayotolewa na wataalamu wa zao hilo kila mwanzo wa msimu.

Landa anasema elimu ambayo hutolewa na maofisa ugani ni namna ya kupanda mbegu, kuchuma maua, kukausha maua kwa kutumia turubai na mikeka pamoja na uhifadhi katika sehemu ambazo hazina unyevunyevu.

Anasema licha ya kilimo hicho kusaidia kukidhi mahitaji yake kiuchumi, bado kuna changamoto ya uhaba wa ardhi ambayo mkulima hulazimika kulima vipande vidogo vidogo.

Mafanikio ya Landa yanaelezwa zaidi na ofisa wa Kampuni ya Pyrethrum Tanzania (PCT) Mussa Malubalo, ambaye anasema wakulima wa Mbeya na Songwe hawajawahi kufikia uzalishaji wa maua yenye sumu yenye kiwango cha 1.97 badala yake walikuwa wanaishia 1.75.

“Tangu tuanze kununua pareto katika mikoa hii (Mbeya na Songwe) hatujawahi kupata maua yenye sumu kali inayofikia kiwango cha 1.97 ambacho kimefikiwa na mkulima huyu,” anasema ofisa wa kampuni inayojihusisha na ununuzi wa zao hilo nchini.

Anasema kwa kutambua na kuthamini juhudi za mkulima huyo, wamempatia cheti cha kumpongeza na kumjengea sehemu ya kukaushia zao hilo ili iwe motisha kwa wakulima wengine kuiga mfano wake.

“Landa amekuwa mshindi wa msimu huu baada ya kuvuna maua yenye kilo 28, mwaka jana mkulima bora alikuwa ni Weston Mwanjokakwa kutoka Kijiji cha Gari Jembe, ubora wa maua ya sumu ilikuwa ni 1.56 wenye kilo 77,” anasema Malubalo.

Pia, anasema kwa mkoa wa Mbeya, mwaka 2018 wakulima 13,000 walizalisha tani 1,904 na walilipwa zaidi ya Sh4.3 bilioni, mtarajio ya mwaka 2019 ni kukusanya tani 2,000.

Mahitaji ya Pareto kwa sasa yameongezeka mara dufu, baada ya nchi za Kenya na Tasmania zilizokuwa zikiongoza kwa uzalishaji wa zao hilo duniani, kupunguza uzalishaji kutokana na kuyumba kwa soko miaka ya 2004 na 2005.

Malubalo anasema licha ya Kenya, Rwanda, Uganda, Tasmania na Papua New Guinea ambazo zinazalisha pareto, duniani bado kuna soko kubwa kwani mahitaji ni tani 20,000 kwa mwaka lakini mavuno katika nchi zote duniani hayafikii tani 10,000 kwa mwaka.

Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima cha Tushishile wilayani Mbeya, Mawazo Ijanga anasema faida ya kilimo cha zao hilo imeanza kuonekana baada ya kuunda vikundi.

Anasema kwamba wakala hufika sehemu iliyopangwa kwa ajili ya kununua bila kuwaibia wakulima tofauti na awali ambako kila mmoja alikuwa anajitafutia soko.

Ijanga anasema kwamba licha ya kilimo hicho kuwa na faida, bado wananchi hawana hamasa ya kuendeleza kilimo cha zao hilo.

“Wananchi wengi wa wilaya ya Mbeya wamejikita katika kilimo cha mahindi na maharagwe ambayo faida yake ni ndogo ukilinganisha na pareto. Serikali inapaswa iwekeze nguvu ya kuhamasisha wananchi kujikita katika zao hilo litakalomkomboa mwananchi na kuongeza pato la Taifa,” anasema Ijanga.

Matumizi ya pareto

Pareto ambayo ilianza kulimwa nchini mwaka 1931, hutumika kutengenezea dawa mbalimbali za kuua wadudu, kampuni nyingi za kutengeneza dawa duniani hutumia sumu ya pareto katika kutengeneza bidhaa zao.

Pia, unga wa maua ya pareto hutumika kuhifadhi nafaka kama vile mahindi na maharagwe ili yasishambuliwe na wadudu waharibifu, lakini hauna madhara kwa binadamu.