Facebook mbioni kuzindua sarafu yake mtandaoni, dunia yapagawa

Dar es Salaam. Kampuni ya Facebook inakabiliwa na upinzani mkubwa kuzindua sarafu yake ya mtandaoni ambayo pamoja na mambo mengine itatumika kulipia matangazo yote yanayofanyika kwenye mitandao yake ya kijamii.

Mwaka huu, ikishirikiana na zaidi ya wabia 20 zikiwamo kampuni za Visa, Mastercard, PayPal, Booking Holdings, eBay, Spotify, Vodafone, Coinbase, Xapo na Uber, imeanzisha mpango wa kuzindua sarafu yake ya mtandaoni itakayoitwa Calibra chini ya taasisi ya Libra.

Lengo la fedha hiyo ni kuwa sarafu ya kwanza rasmi ya kidijitali na itaweza kutumiwa na watumiaji wa Messenger na WhatsApp kote duniani, ikiwaruhusu kutumiana “kwa gharama nafuu na hata bila gharama,” kwa mujibu wa taarifa za Facebook.

Hii itatofautiana na mifumo mingine ya malipo kwa sababu mtumiaji atakuwa akituma fedha wakati anaotaka badala ya kupitia kwanza kuchakatwa katika mifumo ya benki.

Mpango wa Facebook ni kwamba fedha yao iwe mbadala wa fedha za noti na hata kadi za malipo. Wanasema malipo hayo yatafanywa moja kwa moja kutoka katika apps zao.

Pia fedha hiyo ya Libra inaegemea katika sarafu mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na bei kupanda na kushuka. Kukiwa na watu bilioni 1.7 nje ya mfumo wa fedha, lengo la Facebook ni kurahisisha kufanya miamala na kutoa suluhisho la fedha taslimu haraka.

Lakini watunga sera nchini Marekani wanasema sarafu hiyo inaweza ikaharibu mifumo ya kibenki iliyopo katika nchi nyingi endapo itaruhusiwa kutumika kufanikisha miamala tofauti. Kutokana na sababu hizo, kamati mbili za Bunge nchini humo zilimuita na kumhoji mkurugenzi wa sarafu hiyo, David Marcus.

“Naomba niweke wazi, Facebook haitatoa sarafu hii mpaka itakapokamilisha utaratibu wote wa kisheria na kupewa kibali stahiki,” alisema Marcus alipohojiwa hivi karibuni.

Pamoja na maelezo ya mkurugenzi huyo, changamoto iliyopo ni utekelezaji wa alichokisema kwani upo uwezekano wa kutoizindua sarafu hiyo nchini Marekani mpaka utaratibu wa kisheria utakapokamilika ila ukafanyika kwingineko ambako Facebook itaruhusiwa kufanya hivyo.

Sarafu hiyo ya Facebook itakuwa inanunulika kwa fedha za aina 15 tofauti ikiwamo Dola ya Kimarekani, Paundi ya Kiingereza, Euro ya Ulaya na Krona ya Denmark. Kwa sasa, Dola moja ni sawa na vipande 10 vya sarafu hiyo.

Kutumia sarafu hiyo, mteja atatakiwa kuwa na akaunti ya Calibra itakayokuwa kwenye programu maalumu (app) au ikiwa imewekwa kwenye WhatsApp au Messenger.

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, benki na kampuni nyingi za malipo zimerahisisha namna ya kufanikisha miamala kwa kupunguza kama si kuondoa kabisa matumizi ya fedha taslimu.

Miongoni mwa sababu zinazoangaliwa na mamlaka za usimamizi nchini Marekani ambazo huenda zikasababisha kuchelewa kuzinduliwa kwa sarafu hiyo ni uwezekano wa kutumika kutakatisha fedha.

Wataalamu wanaamini Facebook ni dhaifu, hasa katika kukusanya taarifa na kuwajua zaidi ya watu bilioni 2.41 wanaoutumia mtandao huo kila mwezi.

Sarafu za mtandaoni zijulikanazo kama cryptocurrencies, ikiwamo maarufu ya Bitcoin, zilianza kutumika tangu mwaka 2009. Kwa muda wote huo, sarafu hizo hazina udhibiti wa Serikali nyingi duniani.

Wabunge Marekani

Mwenyekiti wa kamati ya huduma za fedha, Maxine Waters anasema watunga sera na mamlaka za udhibiti zinahitaji kujiridhisha na masuala kadhaa kuhusu Libra.

Mwenyekiti huyo alisema wabunge wanahitaji kujiridhisha na mpango mzima kabla ya uzinduzi rasmi.

Mjumbe wa kamati ya benki wa Bunge hilo, Sherrod Brown, amesema Facebook imekuwa na nguvu kubwa, hivyo kuiruhusu iwe na sarafu yake ni jambo linalopaswa kuangaliwa kwa umakini.

“Hatuwezi kuiruhusu Facebook izindue sarafu hii kwa akaunti iliyopo Uswisi bila kujiridhisha,” alikaririwa na BBC English.

Uingereza

Si Marekani tu inayotishwa na sarafu hiyo, Uingereza inajipanga kuchukua hatua kama itaombwa kuruhusu matumizi ya Libra.

Akizungumzia suala hilo, gavana na Benki Kuu ya England, Mark Carney alisema “sarafu yoyote ile inayotakiwa kutumika duniani ni lazima ifuate kanuni na kukidhi viwango vya udhibiti. Endapo Facebook inataka Libra iingizwe kwenye mfumo wa malipo Uingereza, ni lazima iwe chini ya mamlaka ya udhibiti na iwafahamu watumiaji wake.

Kukidhi matakwa ya kikanuni, kampuni za masuala ya malipo zinasema ni suala linalohitaji muda na fedha nyingi kuligharamia.

Suala jingine ni kwamba Libra bado ipo kwenye hatua za kuzinduliwa, hivyo watu wengi hawana taarifa za kutosha.

Nchi za G7

Suala la matumizi ya sarafu ya Facebook pia linawaumiza vichwa viongozi wa mataifa makubwa zaidi kiuchumi duniani (G7) ambao wameazimia kuunda kamati itakayochunguza vihatarishi vyovyote, kama vinaweza kuwepo, endapo itaruhusiwa kuingia kwenye mzunguko wa fedha.

Kamati hiyo, pamoja na mambo mengine, inatarajiwa kuangalia uwezekano wa sarafu hiyo kufanikisha utakatishaji fedha ingawa haijafahamika ni watu wangapi kati ya watumiaji wa mtandao huo watakuwa tayari kuitumia.

Lakini kwa kuzingatia ukubwa wa mtandao huo wa kijamii, watunga sera, wachumi na wataalamu wa masuala ya fedha wanaamini sarafu hiyo ikiingia sokoni itakuwa na ushawishi mkubwa.

Tanzania

Licha ya kuwapo kwa sarafu za mtandaoni zinazotumika maeneo mengi duniani hata nchini, Serikali haizitambui na mara kadhaa imetoa tahadhari.

Taarifa ya majibu ya maswali yaulizwayo mara kwa mara kwa mkurugenzi wa utafiti na sera za uchumi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inasema mfumo wa sarafu ya mtandaoni unajisimamia wenyewe na haudhibitiwi na mamlaka yoyote.

Tangu mwaka 2009 ilipotolewa bitcoin ambayo ni maarufu zaidi, mpaka sasa zipo za aina tofauti zaidi ya 1,600.

“Dhana ya sarafu ya mtandaoni ni mpya na benki kuu nyingi ulimwenguni bado zinafuatilia kwa karibu na kufanya utafiti kuhusu matokeo ya teknolojia hiyo,” inasema BoT.

Taarifa hiyo inaangaliza kuwa ubunifu wa teknolojia unaweza kuboresha huduma za malipo lakini fedha za mtandaoni zinaweza kuchukua nafasi ya fedha zinazotolewa na Benki Kuu hivyo kuziweka Serikali kwenye nafasi ambayo haijawahi kufikirika.

Kutokana na mazingira ya usiri wa muundaji wa sarafu hizo, BoT inashauri wananchi kuwa makini na sarafu hizo.

“Benki Kuu inaendelea kutafiti na kujifunza teknolojia hii kwa kina kwa lengo la kutafuta suluhisho la kudumu ambalo limezingatia mahitaji ya udhibiti wa masuala ya fedha ya nchi,” inasema taarifa hiyo.