Familia ya mwanamke aliyeuawa yaomba msaada kwa Lugola

Muktasari:

Familia ya mwanamke aliyeuawa kikatili baada ya mwanaye kuiba chakula cha jirani imemwomba Waziri Lugola kuingilia kati sakata hilo la mauaji.


Rombo. Familia ya mwanamke aliyeuawa kikatili na wanawake wenzake sita, Adelaide Onesmo mkazi wa kijiji cha Lessoroma, kwa madai ya mwanaye kuiba chakula nyumba ya jirani, wamemuomba waziri wa mambo ya Ndani, Kangi Lugola kuingilia kati sakata hilo.

Wakizungumza na Mcl Digital ,watoto wa marehemu Adelaide wamesema hadi sasa hakuna kinachoendelea na watuhumiwa hawajakamatwa licha ya mtoto aliyehusishwa na tukio hilo, anayesoma darasa la sita, kuonyesha waliohusika na tukio la kumshambulia mama yao kwa kumpiga hadi kufa.

Beatrice Onesmo, mmoja wa watoto wa marehemu, mbali na kuitaka Serikali kuingilia kati lakini alisema tukio hilo si la kwanza kutokea katika familia yao na polisi hawachukui hatua ikiwamo kifo cha baba yao aliyeuliwa kikatili mwaka 2017.

“Haya mauaji ya mama yangu ni ya kusikitisha, na inatuumiza sana sisi familia, hata mwaka 2017 baba yangu mzazi aliuliwa kikatili hivi hivi na waliohusika hawakukamatwa hadi leo tunapoongea licha ya kwamba tupo na jeshi la polisi hapa, hivyo kwa sababu hatuoni kinachoendelea hadi sasa tunaomba Serikali na waziri husika atusaidie,”amesema Beatrice.

Adelaide alipigwa hadi kufa, Februari 11, 2019 kwa madai ya mwanaye kuiba chakula aina ya ngararimo kwa jirani, chakula hicho maarufu kwa wachaga ni mchanganyiko wa maharage na mahindi.