Fatma Karume aeleza sababu kutoonekana hafla siku ya sheria

Muktasari:

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS)  Fatma Karume amesema kitendo cha TLS kutopewa nafasi ya kuzungumza siku ya sheria ni uvunjaji wa miiko ya siku hiyo


Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Fatma Karume ameeleza sababu za kutoonekana katika maadhimisho ya siku ya sheria yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Februari 6, 2019 amedai ni kutokana na mahakama kumzuia asizungumze kwenye hafla hiyo.

Fatma ambaye jana usiku alisambaza katika mitandao ya kijamii hotuba yake aliyopanga kuisoma katika hafla hiyo amesema  kitendo cha mahakama kumueleza kuwa hatotoa hotuba hiyo kililenga kumzuia asihudhurie.

Amedai uamuzi huo umevunja misingi ya miaka 20 ya siku hiyo muhimu ya sheria kwa kukataa kuwasikiliza wanasheria.

“Akufukuzae hakwambii toka, jana nimepata barua kutoka mahakama kwamba muda utakuwa mchache hivyo haitawezekana kutoa hotuba ni wazi kwamba sikutakiwa kuwepo,” amesema.

Katika hotuba yake hiyo Fatma amezungumzia masuala ya ucheleweshwaji wa kesi, hasa akitolea mfano kwa watu wasio na uwezo kwamba wanafuatilia kesi mahakamani ambazo wao ndio wenye haki kwa zaidi ya miaka 15 lakini mpaka wanafariki dunia bado kesi husika haijamalizika.

Februari Mosi, 2019 Fatma Karume alidai  kuna njama za kumzuia kushiriki licha ya kuwa rais wa TLS.

Fatma, mwanaharakati wa sheria, alianzisha madai hayo kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii, akidai kuwa wamepigiwa simu na watu kutoka Ikulu ambao hakuwataja jina na kuambiwa kuwa awasilishe hotuba yake aliyopanga kuisoma siku hiyo, lakini asihudhurie.

Lakini mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Gerson Msigwa amesema madai hayo yanatakiwa kupuuzwa.

“Unataka mimi nithibitishe au nikanushe habari ambazo ziko hewani. Mimi sitafanya hivyo. Mwambieni yeye (Fatma) athibitishe hicho anachodai kinafanyika,” alisema Msigwa.

Katika akaunti yake ya Twitter, Fatma amedai kuwa kuna watu waliojitambulisha kuwa wanatoka Ikulu ambao wanaandaa mipango ya kutaka kuathiri ushiriki na uwepo wake katika sherehe hizo za kila mwaka.

Fatma alidai kuna maofisa waliompigia simu mtendaji mkuu wa TLS, Kaleb Gamaya wakimtaka afikishe ujumbe kwa Fatma kwamba hataruhusiwa kushiriki sherehe hizo.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, Gamaya aliwataka wampigie simu Fatma kumfikishia ujumbe huo, lakini walisisitiza kuwa amfikishie.

Alisema maofisa hao walimpigia tena Gamaya, mara hii wakimwalika Ikulu kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa majaji wapya walioteuliwa na Rais.