Fundi nguo atekwa na wasiojulikana Serengeti

Muktasari:

  • Katika tukio linaloelezwa kuwa la kwanza katika wilaya ya Serengeti fundi wa nguo na muuza vitambaa vya suti katika soko la Mugumu wilayani humo Juma Siki (34) anahofiwa kutekwa na watu wasiojulikana ambao wanaomba kupewa Sh15 milioni ili wamuachie.

Serengeti.  Fundi wa nguo na muuza vitambaa vya suti katika soko la Mugumu wilayani hapa Juma Siki (34) anahofiwa kutekwa na watu wasiojulikana ambao wanaomba kupewa Sh15 milioni ili wamuachie.

Tukio hilo linalotajwa kuwa la kwanza wilayani hapa linadaiwa kutokea Mei 25 nyakati za usiku, Kamanda wa polisi mkoa wa Mara Juma Ndaki amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na wanaendelea na uchunguzi wa kina.

Amesema wanafuatilia kubaini wahusika kupitia simu ya Juma ambayo imetumika kutuma ujumbe kwa rafiki yake ukimtaka atumiwe Sh15 milioni ndipo wamuachie huku ukieleza kuwa bado yupo hai.

Amesema ndani ya gari ya Juma aina ya Toyota Noah lililokutwa karibu na nyumba yake walikuta damu, kisu, mawe na vitu vingine ambavyo inadaiwa vilitumiwa na watuhumiwa wa tukio hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu amesema tukio hilo limewastua na askari wanaendelea na ufuatiliaji na ameomba watu wenye taarifa sahihi wasaidie ili watuhumiwa waweze kukamatwa.

Sirikwa Marwa aliyedai ni rafiki mkubwa wa  Juma amekiri kupokea ujumbe wa simu kupitia namba ya rafiki yake ukimtaka ajitahidi kutuma kiasi hicho cha fedha.

"Katika ujumbe huo hajaelekeza tunazipata wapi, bali unadai tutume kiasi hicho kwenye namba hiyo ya mtandao wa Vodacom, baada ya hapo haipatikani tena," amesema.

Baadhi ya wananchi wameomba uchunguzi ufanyike wa kina kwa kuwa mazingira ya tukio yanaibua hofu kwa wakazi wa mji huo.