Fungia fungia magazeti yaibuka bungeni

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Devotha Minja akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Baadhi ya wabunge wamehoji uamuzi wa Serikali kuyafungia magazeti yanayoonekana kuandika habari nzuri zisizoipendeza Serikali.

Dodoma. Mbunge wa Viti maalum (Chadema), Devotha Minja na mwenzake wa (Konde) wa CUF, Khatib Said Haji wamehoji sababu za Serikali ya Tanzania kuyafungia magazeti yanayoandika habari zisizopendezwa nazo, huku Devotha akiinyooshea kidole  Idara ya Habari Maelezo kuwa imegeuka kitanzi cha wanahabari nchini.

Wametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 18 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mwaka 2019/2020 ya Sh30.8 bilioni.

Wabunge hao walirejea hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kuwa hadi kufikia Machi 2019 magazeti yaliyopewa leseni  tangu Sheria mpya ya Huduma za Habari ilipoanza kutekelezwa mwaka 2017 ni 216 na 42 ni ya sekta ya umma na 184 ya sekta binafsi, wakieleza hiyo si hoja kwa kuwa yanabanwa na kufungiwa.

“Nimemsikia Waziri (Dk Harrison Mwakyembe) akisema idadi ya magazeti tuliyonayo sijui na redio. Hoja si kuwa na vyombo vingi vya habari, hoja ni vinafanya kazi kwa uhuru? Au ndio zile ambazo waziri akiamka asubuhi anafungia kwa sababu hayajaandika habari fulani.”

“Habari maelezo hivi sasa imegeuka kitanzi cha wanahabari. Ukienda katika vyumba vya habari utakuta fomu kibao wameandikiwa na Maelezo wakitakiwa kujieleza kwa nini wasifungiwe,” amesema Devotha.

Amesema idara hiyo badala ya kuelekeza vyombo vya habari vifanye nini, imegeuka na kuyafungia magazeti yanayoandika habari nzuri ambazo haziipendezi Serikali, huku akihoji sababu za habari kukosewa lakini kinafungiwa chombo cha habari badala ya kushughulika na mwandishi husika.

“Maana yake ni nini maana yake ni vyama vya upinzani visifanye mikutano na wanahabari, mnavitaka vyombo vya habari vifanye kazi za Serikali,” amesema Devotha.

Kwa upande wake, Khatib amesema: “Juzi nilimsikia Waziri wa Mambo ya Nje (Profesa Palamagamba Kabudi) akisifia nchi yetu kutokana na kupata sifa ya uhuru wa vyombo vya habari na moja ya eneo alilosema ni Tanzania kuwa na magazeti mengi.”

“Mkurugenzi wa maelezo juzi tu ameyataka magazeti yaende kujieleza kwa kuandika habari za kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo aliyeichambua taarifa ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali). Vyombo hivi vilikuwa na haki ya kuhabarisha habari hii lakini vimetakiwa kwenda kujieleza,” amesema Khatib.

Khatib amesema wakati huo huo kuna magazeti yanaandika habari za kuwadhalilisha watu lakini hayachukuliwi hatua yoyote: “Kwanini hawaitwi wapo nyuma ya nani?, wapo wengine wakitoa maoni kidogo tu wanashtakiwa.”