GGM kurahisisha upatikanaji mkaa mbadala

Makamu wa Rais  wa Kampuni ya AngloGold Ashanti, GGM, Simon Shayo  (wa pili kushoto) akitoa mada katika mjadala wa Jukwaa la Frika lililojadili matumizi ya mkaa, uchumi na mazingira yetu, jijini Dar es Salaam . Picha na Said Khamis

Muktasari:

AngloGoldAshanti ni miongoni mwa kampuni zilizodhamini mdahalo wa Mwananchi Jukwaa la Fikra ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa ushirikiano na vituo vya ITV/Redio one uliofanyika Februari 7 katika ukumbi wa Kisenga, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kisingizio kikubwa cha baadhi ya watu kushindwa kutumia mkaa mbadala ni kutoupata kwa wakati, gharama kubwa na wakati mwingine kutamani kuutengeneza lakini wanakosa vitendea kazi.

Jambo hilo limewafanya wakazi wa vijiji mbalimbali kuendelea kutumia kuni pamoja na mkaa kama nishati kuu ya kupikia kwa sababu hupatikana kwa urahisi.

Kwa kulitambua hilo, uongozi wa kampuni AngloGoldAshanti inayomiliki mgodi wa ghahabu wa Geita, GGM ipo katika mchakato wa kuviwezesha vikundi mbalimbali kutoka vijiji 16 kwa kupata mashine za kutengenezea mkaa mbadala.

Mpango huo utakuwa ahueni kwao kwa sababu utawawezesha wananchi kuondokana na tatizo la kutopatikana kwa mkaa mbadala na hivyo kupunguza matumizi ya kila siku ya kuni na mkaa.

Mkaa mbadala hutengenezwa kwa kutumia malighafi tofauti, lakini mpango huo wa GGM unalenga mkaa unaotokana na pumba za mpunga na makapi ya kahawa.

AngloGoldAshanti ni miongoni mwa kampuni zilizodhamini mdahalo wa Mwananchi Jukwaa la Fikra ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa ushirikiano na vituo vya ITV/Redio one uliofanyika Februari 7 katika ukumbi wa Kisenga, Dar es Salaam.

Kijitonyama Dar es Salaam

Mdahalo huo wa tatu, ulikuwa na mada ya ‘Mkaa, Uchumi na Mazingira yetu’ ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa mazingira akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba aliyekuwa mgeni rasmi.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu, Makamu wa Rais wa AngloGoldAshanti, Simon Shayo anasema wamefikia hatua ya kuviwezesha vikundi hivyo ili kuunga mkono mkono jitihada za Serikali za kulinda na kuhifadhi mazingira, pamoja na kupunguza matumizi ya mkaa na kuni.

Shayo anasema wana mpango wa majaribio unaolenga kuwasaidia wanakijiji kupitia vikundi vyao kwa kuwapa mashine zitakazotengeneza mkaa mbadala unaotokana na malighafi mbalimbali ikiwemo ya pumba za mpunga.

“Tayari tuna vikundi tunavyofanya navyo kazi kupitia kilimo cha mpunga ambavyo vinatoka vijiji 16 na mitaa 18 inayozunguka mgodi wetu,” anasema.

“Mpango huu wa majaribio unatarajia kukamilika katikati ya mwaka huu, tumeamua kufanya hivi ili tuone mwitikio wa wananchi kwa sababu unaweza ukafanya jambo zuri kwa wananchi, lakini wenyewe wasilipendi ndio maana tunafanya mpango huu wa majaribio.

“Ila nawaambia mkaa huu mbadala utauuzwa kwa bei ambayo kila mtu anaweza kuimudu. Mkaa huu mbadala utachukua nafasi ya mkaa wa miti na utapunguza matumizi ya kuni na mkaa ili kuilinda misitu yetu.”

Shayo anasema uhaba wa vyanzo mbadala vya nishati na uvunaji usioendelevu wa miti na mazao yake kwa ajili ya kutengeneza mkaa ni sababu mojawapo inayochangia kuharibu mazingira.

Anafafanua kuwa maeneo ya vijijini mkaa na kuni ndivyo vyanzo pekee vya nishati, “lakini ukiyatazama kwa ukaribu maeneo (hayo) utagundua kuna rasilimali nyingi ikiwemo pumba za mpunga zinazoweza kugeuzwa kuwa nishati mbadala.”

Kuhusu mdahalo wa Jukwaa la Fikra, Shayo aliupongeza uongozi wa MCL akisema ingawa umechelewa, lakini ni mwanzo mzuri uliofanywa na kampuni hiyo kujadili mada hiyo.

“Ni mwanzo mzuri kwa sababu unaleta wadau mbalimbali kutoka ngazi za juu na chini wanaochangia na kuchagiza sera za sekta hii. Mjadala huu lazima ushuke katika ngazi ya jamii kwa sababu huko ndiko wanatumia mkaa na kuvuna miti kwa ajili ya kuni na kutengeneza mkaa.”

Anasema, “hili linatakiwa lifanyike kwa mapana yake na watu waunganishe matumizi sahihi ya mkaa, mazingira na maisha yao ya kila siku.”

“Ni vyema tuunganishe matumizi ya mkaa, uvunaji holela wa miti na tujue isipotuathiri sisi basi vizazi vijavyo.”

Shayo anasisitiza kuwa nishati mbadala ni lazima iangaliwe kwa mapana huku akitolea mfano matumizi ya gesi mijini.

Anasema kwamba sio watu wote wanaoishi maeneo hayo wanamudu kutumia gesi kwa sababu hakuna uchambuzi kina uliofanyika, badala yake baadhi yao wana imani kuwa nishati hiyo bado ni gharama.

“Ukiangalia uchafu unaotokana na mkaa na uhifadhi wake ulivyokuwa mgumu, ukilinganisha na athari zake kwenye mazingira watu wengi wangetumia gesi, lakini sasa hivi hata mtumishi wa umma akiwa anarudi safari anabeba gunia la mkaa,” anasema makamu huyo wa rais wa AngloGoldAshanti.

Uhifadhi wa mazingira

Mbali na hayo, Shayo anasema katika shughuli zao za uchimbaji wanaheshimu uhifadhi wa mazingira na ni miongoni mwa maeneo wanayoyapa kipaumbele.

Anasema kutokana na shughuli zao wameweka mfumo wa kusimamia mazingira ambao wanahakikisha unazingatiwa katika shughuli zao za kila siku mgodini.

Miongoni mwa mambo wanayoyafanya katika mfumo huo ni upandaji wa miti ya asili wakishirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ikiwa ni sehemu mojawapo ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhifadhi mazingira.

“Ni nadra sehemu ya mgodi kuwa na msitu wa asili, lakini sisi tumefanikiwa kwa kufanya urejeshaji wa miti ya asili baada ya kufanya uchimbaji wa madini,” anasema Shayo.

Hata hivyo, eneo la msitu wanalolihudumia limekuwa likivamiwa mara kwa mara na wananchi wanaozunguka mgodi kwa kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na kutengeneza kuni.

“Tunafanya jitihada mbalimbali za kudhibiti vitendo hivyo ikiwamo kufanya doria mara kwa mara kwa kutumia helkopta tukishirikiana na uongozi wa mkoa. Tunaendelea kuelimisha jamii namna ya kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ili kulinda misitu na mazingira.”

Makamba aeleza madhara matumizi mkaa

Katika mdahalo huo, Makamba ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli, alisema watu 22,000 hufariki dunia hapa nchini kila mwaka kutokana na athari za matumizi ya mkaa na kuni.

Mbali na hilo, alisema mtu akivuta moshi unaotokana na matumizi ya mkaa na kuni anakuwa katika hatari kubwa ya kiafya.

“Gharama za kiafya kutokana na uharibifu wa hewa unaotokana na mapishi ya kuni na mkaa ni Dola 1.8 milioni za Marekani kwa mwaka,” alisema Makamba.

Hata hivyo, alisema Serikali imenufaika na Jukwaa la Fikra na kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na wadau na kwa kuanzia wataunda timu itakayojadili masuala hayo serikalini.