UCHOKOZI WA EDO: Ghafla mlima Kitonga ukanifikirisha CAG na masaibu yake

Monday January 14 2019Edo  Kumwembe

Edo  Kumwembe 

By Edo Kumwembe

Siku za mwisho za likizo yangu, Ijumaa nilienda Iringa kufanya utalii wa ndani. Kumbe nchi yetu ina vivutio vingi vya utalii kuliko vinavyozungumzwa. Inavutia sana.

Nikakumbana na kituko fulani cha kufurahisha pale mlima Kitonga. Mlima maarufu zaidi kwa waendao nyanda za juu kusini. Barabara nyembamba imechongwa kando ya mlima mrefu wenye kona unaopandisha kuelekea nyanda za juu kusini.

Nilikuwa naendesha nikitumia akili ya kuzaliwa. Kifupi niliamua kutumia akili za mbayuwayu. Namba moja wetu wa zamani, JK aliwahi kutuambia wakati mwingine tutumie akili zetu za kawaida kisha tuchanganye na zile za kuambiwa.

Katikati ya mlima nikakutana na malori makubwa yanayokwenda nje ya nchi yakiwa yamebeba shehena za mizigo, nadhani ni kutoka bandarini Dar es Salaam. Ni mazito kwelikweli. Mara nyingi hupata ajali kwa kurudi nyuma kwa sababu yanashindwa kupandisha mlima Kitonga.

Nikatumia akili za JK. Nikalipita lori la kwanza. Bado mbele yangu kulikuwa na malori mengine ambayo yalinitabirisha kifo changu kama yangeshindwa kupanda na kurudi nyuma kwa kasi. Ningeweza kuwa marehemu muda wowote. Nikaanza kuyapita au kwa ‘Kiswahili cha Kiingereza’ tunaweza kusema kuovateki.

Nilipomaliza mlima Kitonga trafiki akalipiga mkono gari langu. Kosa? Nikaambiwa nimeovateki katikati ya mlima. Ni kosa kwa sasa, haturuhusiwi. Nikahoji, sawa haturuhusiwi, lakini lori likishindwa kupanda halafu likaja kulalia gari langu dogo na kunifanya marehemu? Nadhani tukio kama hilo likitokea dereva wa lori hatakuwa na kosa kubwa. Kama akipata bahati ya kuwa hai basi anatozwa faini tu.

Nikapigwa faini nikaondoka zangu. Ghafla tukio lile nikalifananisha na hili la CAG wetu. Yule Mzee Profesa. Anajaribu kulikwepesha taifa katika ajali lakini yeye ndiye anasakwama. Amejiwa juu kwelikweli na mkuu wa mhimili pale Dodoma.

Sasa anaandikwa vibaya na baadhi ya magazeti. Tatizo amekuwa yeye anayejaribu kuhakikisha Taifa linakwepa ajali. Nilidhani tungejadili alichosema, watu wanaanza kumjadili yeye. Hili ndio tatizo la mwafrika. Yule trafiki alijaribu kunijadili mimi badala ya kukusanyika na wasimamia sheria wenzake kujadili uwezekano wa lori kurudi nyuma ghafla na uzito wake kisha kulivaa gari dogo. Ni ngumu kwelikweli kwa ufisadi kumalizika nchini.

Advertisement