Gondwe, kutoka kufanya usafi hadi u-DC

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe

Muktasari:

  • Gondwe aliyezaliwa mkoani Mwanza, anasema matamanio yake ya kupata elimu ya juu ndiyo sababu ya kufanya kazi ya usafi hospitali na uhudumu hotelini ili apate fedha za kufika huko.

Dar es Salaam. Wahenga walisema “mvumilivu hula mbivu”. Pengine kauli hiyo inasadifu maisha aliyopitia mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe ambaye simulizi ya mafanikio ya maisha yake inaanzia alipoajiriwa Hospitali ya Bugando mjini Mwanza kufanya kazi ya usafi.

Gondwe aliyezaliwa 1974 alifahamika zaidi alipokuwa mtangazaji wa kituo cha televisheni cha ITV kilichopo jijini Dar es Salaam, lakini kabla ya hapo alianzia Redio Free Africa (RFA) ya jijini humo.

Hivi sasa ni msomi wa kiwango cha shahada ya pili katika mawasiliano ya umma na kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tumaini kilichopo jijini Dar es Salaam.

“(Vijana wengi) wanafikiri nimetoka katika familia bora na kusoma bila shida mpaka kufikia hatua hii, lakini wacha niwaambie siku zote usikubali ndoto yako ife kwa kisingizio chochote kile,” anasema Gondwe katika mahojiano na Mwananchi.

Anasema uvumilivu wake na kutokata tamaa ndivyo vilivyomuongoza kufikia mafanikio katika maisha aliyonayo kwa sasa.

Mbali na kufanya shughuli za usafi hospitali, pia aliwahi kuwa mhudumu katika hoteli ya kitalii ya Mwanza.

Gondwe aliyezaliwa mkoani Mwanza, anasema matamanio yake ya kupata elimu ya juu ndiyo sababu ya kufanya kazi ya usafi hospitali na uhudumu hotelini ili apate fedha za kufika huko.

“Kila mmoja alinishangaa, lakini hilo halikunirudisha nyuma wala kusababisha nikate tamaa, badala yake niliwaomba wazazi wangu wanipeleke kidato cha sita.”