HUKUMU YA MA-DED: Mchuano wa wanasheria

Dar es Salaam. Mvutano wa tafsiri ya kisheria miongoni mwa wanasheria, umeibuka baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Aderladus Kilangi kusema wakurugenzi wa halmashauri za majiji, miji/wilaya na manispaa wataendelea kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hadi utakapotolewa uamuzi mwingine.

Mkinzano wa kisheria wa wanasheria hao umetokana na hatua ya Serikali kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Ijumaa iliyopita. Katika hukumu hiyo, jopo la majaji watatu, Dk Atuganile Ngala (kiongozi wa jopo), Dk Benhajj Masoud na Firmin Matogolo ilisema watendaji hao kusimamia uchaguzi kunakinzana na matakwa ya Katiba inayotaka NEC iwe huru na kubatilisha kifungu cha 7(3) kinachoipa Tume mamlaka ya kumteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa msimamizi wa uchaguzi.

Hukumu hiyo ya Mahakama Kuu ilitokana na kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na watetezi na wanaharakati wa haki za binadamu na demokrasia kwa kushirikiana na vyama vya siasa, wakiwakilishwa na mwanachama wa Chadema, Bob Wangwe.

Akizungumzia hatua ya AG jana, Fatma Karume, mwanasheria kutoka kampuni ya Immma ambaye alikuwa wakili wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo alisema haina mashiko kisheria.

Alisema kwa mujibu wa sheria, kitendo cha kukata rufaa kinaweza kusimamisha utekelezaji wa hukumu ya Mahakama Kuu pale itakapokuwa sheria haina athari endelevu. Alisema sheria iliyobatilishwa na Mahakama inaendelea kuvunja Katiba, hivyo ina athari endelevu na kukata rufaa hakutoshi kusema kuwa hiyo sheria itatumika.

“Nitampeleka Mahakamani kwa kuvunja amri ya Mahakama, siyo kazi yangu kumfundisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali sheria, ninangoja hukumu na nyaraka mbalimbali, nitakutana naye mbele kwa mbele mahakamani. Sina ugomvi naye, siwezi kumfundisha kazi yake, atafundishwa na Mahakama,” alisema Fatma.

Alisema ni kitu kibaya Mwanasheria Mkuu kupelekwa mahakamani kwa kuvunja hukumu ya Mahakama, “ninachotaka wafuate sheria, hukumu ya Mahakama ikitolewa waifuate, hilo ndilo jambo ninalotaka, sasa binafsi siwezi kuwaeleza, ila Mahakama itafanya kazi yake.”

Hata hivyo, mwanasheria kutoka kampuni ya Avis Legal, Hamza Jabir alisema kwa kipindi hiki ambacho Mahakama Kuu imetoa mapendekezo yake, kifungu cha 71 na 73 kitaendelea kutumika, “mabadiliko ya sheria hiyo yatafanyika pale mamlaka zinazohusika zitakapopeleka mambo hayo kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya sheria. Mahakama kazi yake ni kutafsiri sheria ili mabadiliko yafanyike, inabidi hivyo vifungu vipelekwe bungeni,” alisema Jabir.

Alisema vifungu hivyo vitaendelea kuwapo kama vilivyo hadi suluhisho litakapopatikana ama kufanyiwa mabadiliko au kuondolewa kabisa.

“Kama hukumu ingebaki kama ilivyo, yaani isingekatiwa rufaa ina maana kungefanyika mabadiliko ya hivyo vifungu vya Katiba, lakini kwa sababu hilo halijafanyika, kila kitu kitabaki kama kilivyo.

Lakini, wakili wa kujitegemea, Sinare Zaharani alisema kwa kawaida ikitokea kuna uamuzi wa Mahakama Kuu halafu ukakatiwa rufaa, utekelezaji wake huwa unaombewa maombi ya kuyasitisha kutekelezwa.

“Wewe uliyeshinda kesi unaweza kwenda mahakama kuu kukazia hukumu, lakini wa upande wa pili naye akaenda pia kuomba kutokukazia hukumu, ambayo inategemea na asili ya hukumu iliyotolewa.

“Katika hukumu ya kesi hii, unataka ile itekelezwe huwezi kwenda mahakamani kuwasilisha maombi ya kukazia huku, bahati nzuri sheria yenyewe inasema kwamba iwapo mahakama kuu itataja kifungu fulani kinachokinzana na Katiba, Serikali hupewa muda fulani wa kufanya mabadiliko.”

Alisema iwapo Serikali haikufanya hivyo kwa muda fulani hapo ndiyo hukumu itakuwa imepitishwa.

“Anachokisema AG kwa mujibu wa sheria ndicho kitakachofanyika ikitokea kuna uchaguzi itakayotumika ni ileile,” alisema Zaharani.

Hata hivyo, mhadhiri wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Dk Kevin Mandopi alisema hukumu yoyote ikitolewa Mahakama inaiwekea zuio ile ya kwanza hadi itakapotenguliwa.

“Kwa mujibu wa taratibu za kisheria, inayosimama sasa ni ile hukumu ya mara ya mwisho,” alisema, “kama mtu alifanya kosa la jinai akatiwa hatiani na Mahakama ya chini na akahukumiwa kifungo, lakini akakata rufaa, atapelekwa gerezani, hadi pale hukumu yake itakapotenguliwa na Mahakama nyingine kwenye ngazi ya rufani.”