HakiElimu yazoa tuzo Afrika

Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara, akiwa na maofisa waandamizi wa serikali wa elimu na Mkurungezi Mtendaji wa HakiElimu, Dk John Kalage wakinyanyua glasi za 'Champagne' kusheherekea ushindi HakiElimu kama NGO inayofanya vizuri Afrika.

Muktasari:

Shirika la Hakielimu limekuwa mshindi wa jumla wa tuzo za asasi za kiraia Afrika kutokana na shughuli zake kwenye sekta ya elimu

Dar es Salaam. Shirika la Hakielimu limekuwa mshindi wa jumla wa tuzo za asasi za kiraia Afrika kutokana na shughuli zake kwenye sekta ya elimu.

Mkurugenzi wa Haki Elimu,  Dk John Kalage amesema tuzo hiyo inayoitwa 'The African Civil Society Excellence Awards 2019' iliyotolewa na 'Epic Africa' ilishindaniwa na asasi zaidi ya 300 kutoka katika nchi 46 barani Afrika.

Akizungumza leo Jumatatu Mei 20, 2019 katika hafla fupi ya kusherehekea ushindi huo,  Dk Kalage amesema awali walishinda katika vipengere vitatu kikiwemo cha uwazi na uwajibikaji kabla ya kutwaa tuzo ya jumla.

"Ushindi huu sio wetu peke yetu, tuzo hii ni ya Tanzania ukweli ni kwamba ushindi huu usingewezekana bila ushirikiano baina ya Serikali, jamii na mashirika mengine ya kiraia," amesema Dk Kalage.

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Witara amesema Haki Elimu wametimiza wajibu wao katika kuhamasisha ubora wa elimu Tanzania huku wakisaidia kutatua baadhi ya changamoto.

"Kwa hiyo tuzo hii sio tu heshima kwenu, ni heshima kwa Tanzania ndio maana Serikali tupo hapa," amesema Waitara.

Amesema awali HakiElimu ilionekana kama taasisi ya kunyoshea vidole changamoto za kielimu lakini sasa pamoja na kuibua changamoto hizo inasaidia kutatua.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard  Akwilapo amesema wizara hiyo inatambua mchango wa HakiElimu kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

"Tuzo hii imeenda sehemu sahihi kutokana na mchango wenu katika kukuza sekta hii, Serikali inatambua juhudi za mashirika yasiyo ya kiserikali na tutaendelea kushirikiana," amesema Dk Akwilapo.