Hakimu adai kesi ya ‘Mpemba wa Magufuli' inamtesa

Muktasari:

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema anataka kuona kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Yusuf Ali maarufu ‘Mpemba wa Magufuli' na wenzake watano inafikia mwisho kwani imekaa muda mrefu

Dar es Salaam. Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili Yusuf Ali maarufu ‘Mpemba wa Magufuli' na wenzake watano inamtesa kutokana na kutofikia mwisho.

Hakimu Simba amesema hayo leo Jumatatu Machi 11,2019 wakati upande wa utetezi ukiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kutumia nguvu katika kupata hatima ya kesi hiyo.

Yusuf na wenzake watano, wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6 milioni.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali, Candid Nasua kudai shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.

"Anayeendesha shauri hili ni Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja (Nchimbi) kwa sasa yupo nje ya mahakama hii anafanya majukumu mengine tunaomba tarehe nyingine kutoa hali halisi ya shauri hilo," alidai Nasua

Wakili wa utetezi, Neemia Nkoko amedai rekodi zinaonyesha tangu mwaka 2017 upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo wameshangazwa kusikia upande wa mashtaka kuwa upelelezi bado haujakamilika.

"Tunaiomba mahakama hii itumie nguvu tunachotaka kujua hatma ya watu wetu na rekodi zipo tangu mwaka juzi zinaonyesha upelelezi umekamilika halafu leo hii mnatuambia eti upelelezi haujakamilika, inashangaza sana," amedai Nkoko.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema rekodi zinaonyesha Oktoba 23, 2018 upande wa mashtaka ulidai upelelezi umekamilika hivyo aliwataka upande wa mashtaka wamueleze Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi kukamilisha.

"Hili shauri linatutesa sana tunaulizwa kuna tatizo gani kwa kuwa hatutakiwi tuwe nalo hadi leo hii, hii kesi ipo tangu mwaka 2016 hivyo nawaagiza mumwambie Nchimbi ile kauli aliyoitoa imefikia wapi maana inatugombanisha na hawa washtakiwa," amesema Simba.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 25, 2019 itakapotajwa tena na washtakiwa wote wamerudishwa rumande kwa kuwa mashtaka yao hayana dhamana.