Hakimu akwamisha kesi ya Mdee

Muktasari:

  • Kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli inayomkabili Mbunge wa Kawe, Halima Mdee imeshindwa kuendelea na ushahidi kutokana na hakimu anayeendesha shauri hilo kupata udhuru.

Dar es salaam. Kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli inayomkabili Mbunge wa Kawe, Halima Mdee imeshindwa kuendelea na ushahidi kutokana na hakimu anayeendesha shauri hilo kupata udhuru.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patric Mwita leo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa kesi hiyo ilikwenda mahakamani hapo kwa ajili ya kusikilizwa na kuomba iahirishe kwa kuwa hakimu anayeendesha shauri hilo amepata udhuru

"Upande wa mashtaka tunae shahidi Abdi Chembeya lakini kutokana na hakimu anayeendesha shauri hili kupata udhuru tunaiomba Mahakama ipange tarehe nyingine,” alisema.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi aliahirisha shauri hilo hadi Mei 15 na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Mpaka sasa  mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi katika kesi hiyo akiwamo mkuu wa kituo cha polisi Urafiki, Mrakibu wa Polisi (SP), Batseba Kasanga.

Katika kesi hiyo, Mdee anadaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni alitamka maneno dhidi ya  Rais Magufuli kuwa:  “Anaongea hovyo, anatakiwa  afungwe breki,” kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kuhatarisha uvunjifu wa amani.