Hakimu atishia kuifuta kesi ya Wema Sepetu

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa ahirisho la mwisho kwa upande wa mashtaka katika kesi ya kuchapisha video ya ngono inayomkabili msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu(30) kuhakikisha unapeleka mashahidi wa kutosha, vinginevyo kesi hiyo itafutwa.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa ahirisho la mwisho kwa upande wa mashtaka katika kesi ya kuchapisha video ya ngono inayomkabili msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu (30) kupeleka mashahidi wa kutosha, vinginevyo kesi hiyo itafutwa.

Wema ambaye alikuwa Miss Tanzania mwaka 2006  anakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha video ya ngono na kusambaza katika mtandaoni wa kijamii wa Istagram kinyume cha sheria.

Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Aprili 18, 2019 na Hakimu Mkazi, Maira Kasonda baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama kuwa shahidi aliyetakiwa kutoa ushahidi yupo mkoani Morogoro kikazi.

"Natoa ahirisho la mwisho, upande wa mashtaka tarehe ijayo kama mtakuwa hamna shahidi muiondoe kesi hii mahakamani hapa au vinginevyo mimi nitaifuta," amesema Hakimu Maira.

Hii ni mara ya pili kwa kesi hiyo kushindwa kuendelea mahakamani hapo ikiwa katika hatua ya ushahidi, kwani Machi 18, 2019 iliahirishwa kutokana na upande wa mashtaka kukosa shahidi.

Awali, wakili wa Serikali, Gloria Mwenda alieleza kesi hiyo ilikwenda mahakamani hapo kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi lakini shahidi ambaye walimtegemea kutoa ushahidi yupo mkoani Morogoro kikazi.

Gloria amemtaja shahidi huyo kuwa ni Frank Bizuro ambaye ni ofisa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Hakimu Kasonde baada kupitia maelezo ya upande wa mashtaka, aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 14, 2019 kesi hiyo itakapoendelea.

Wema alifikishwa  kwa mara ya kwanza Kisutu  Novemba Mosi mwaka jana kujibu shtaka hilo. Hata hivyo, mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana.

Katika kesi ya msingi, Wema anadaiwa Oktoba 15 mwaka jana katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam alichapisha video ya ngono na kuisambaza katika mtandaoni wake wa kijamii wa Instagram.

Hata hivyo, siku alivyosomewa maelezo ya awali, Wema alikubali kuwa  yeye anakaa Mbezi Salasala na anamiliki mtandao wa kijamii wa Istagramu wenye jina la Wemasepetu.

Katika maelezo hayo ya awali, Wema alikana kurekodi  video ya ngono ambayo haina maudhui kupitia simu yake ya kiganjani.

Alikiri kukamatwa Oktoba 29 mwaka jana kwa tuhuma hiyo na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central) kwa ajili ya kuhojiwa.

Pia  alikubali kuwa alifikishwa Mahakama ya Kisutu Novemba Mosi, 2018, kujibu shtaka linalomkabili.

Lakini alikana kusambaza video hiyo katika akaunti yake ya Istagram.