Hakimu kesi ya ‘Mpemba’ aliyetajwa na Magufuli ahoji upelelezi kutokamilika

Muktasari:

Hakimu wa kesi ya Yusuf Ali maarufu ‘Mpemba wa Magufuli’ amehoji sababu za upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika na kuutaka upande wa mashtaka kutoa majibu Desemba 18

 


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeutaka upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Yusuf Ali maarufu ‘Mpemba wa Magufuli',  kutoa majibu ya kueleweka juu ya upelelezi washauri hilo umefikia wapi Desemba 18.

Katika kesi hiyo, Yusuph  na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manne, ikiwamo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6 milioni.

Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

"Nawapa nafasi ya mwisho upande wa mashtaka hadi Desemba 18. Nataka mje na majibu upelelezi wa kesi hii  umefikiwa hatua gani? haiwezekani ichukue muda mrefu kukamilika upelelezi,” alisema  Hakimu Simba.

Awali,  Wakili wa Serikali,  Elia Athanas aliieleza Mahakama kuwa kesi hiyo ilikwenda kwa ajili ya kutajwa na kwamba uandaaji wa nyaraka zote ambazo ni uendeshaji wa shauri pamoja na uchujaji wa washtakiwa upo katika hatua nzuri.

"Upelelezi wa shauri hili umefikia katika hatua nzuri, uandaaji wa nyaraka zote muhimu ambazo ni uendeshaji na usikilizaji wa shauri hili pamoja na uchujaji wa washtakiwa upo katika hatua za mwisho. Tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," alisema Athanas.

Wakili Athanas baada ya kueleza hayo,  wakili wa utetezi Aloyce Komba alihoji ni nyaraka gani hizo na zimefika hatua gani.

Akijibu, Athanas alisema ni nyaraka  za uendeshaji na usikilizaji wa shauri hilo pamoja na uchujaji wa washtakiwa kabla ya kuwasomwa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 18  itakapotajwa tena.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika tarehe tofauti kati ya Januari 2014 na Oktoba, 2016 wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, washtakiwa wanadaiwa kujihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza  vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh392.8 milioni bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.

Katika shtaka la pili inadaiwa kuwa Oktoba 26, 2016 wakiwa Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 13.85 vikiwa na thamani ya Dola za Marekani 30,000 (Sh 65.4 milioni ).

Oktoba 27, 2016 wakiwa Tabata Kisukuru washtakiwa hao wanadaiwa walikutwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 11.1 vikiwa na thamani ya Dola za Marekani 15,000 (Sh 32.7 milioni).

Pia inadaiwa Oktoba 29, 2016 walikutwa na vipande 36 vyenye thamani ya Sh294.6 milioni bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.